Katika kukabiliana na mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa wa virusi vya Marburg nchini Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU) umetenga TZS 396.2 milioni (€150,000) kama msaada wa kibinadamu ili kusaidia juhudi za taifa katika kudhibiti kuenea kwa virusi hivi hatari, ambavyo vinahatarisha zaidi ya watu milioni 2.98.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya jana imesema mradi huu wa dharura utaendelea kwa miezi minne hadi mwisho wa Mei 2025, ukilenga kuwafikia zaidi ya watu milioni 1.47 katika mkoa wa Kagera.
Fedha hizi kutoka EU
zitaimarisha juhudi za Shirika la Msalaba Mwekundu la Tanzania katika utoaji wa
msaada muhimu, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, uhamasishaji wa usafi,
ushirikishwaji wa jamii, na mawasiliano ya hatari.
Juhudi hizi
pia zitajumuisha hatua za ujumuishi kwa ajili ya makundi maalum kama wazee na
watu wenye ulemavu.Tanzania ilithibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa Marburg katika
Mkoa wa Kagera tarehe 20 Januari 2025.
Huu ni
mlipuko wa pili wa ugonjwa huo nchini, baada ya ule wa mwaka 2023 katika mkoa
huo huo, imesema taarifa hiyo ya EU.
EU imesema msaada huu ni
sehemu ya mchango wa jumla wa EU kwa Mfuko wa Dharura wa Kukabiliana na Majanga
(DREF) wa Shirikisho la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC).
Mlipuko huu unaleta changamoto zaidi kutokana na mwingiliano wa watu kupitia mipaka, hali inayoongeza haja ya msaada wa vifaa na uratibu.
Wakati huo huo, Tanzania inakabiliana na
changamoto zingine za afya ya umma, ikiwemo mlipuko wa Mpox katika mikoa 10 na
kipindupindu katika mikoa yote 31.
0 Maoni