Jeshi la Polisi mkoa wa
Mwanza limewataka wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi mkoani humo kufuata
sheria kwa kuwasimamia vyema askari wanaowaajiri kufanya kazi ya ulinzi katika
maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Sarige kwenye kikao kazi na wamiliki hao
ndipo akawahimiza kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kutoa mafunzo kwa
walinzi ili kuleta uelewa wa pamoja na kuimarisha nidhamu kwa askari hao wakati
wanapotekeleza majukumu ya ulinzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi
Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Yesaya
Suddy akitoa elimu katika kikao hicho amesema katika jamii si ajabu kukutana na
mlinzi anayelinda mali yenye thamani ya zaidi milioni mia tano lakini hajui
hata kutumia silaha aliyonayo kwenye lindo kitu ambacho ni hatari kwa usalama.
Naye, Mwenyekiti wa Chama
cha Ulinzi Rasilimali Watu Kanda ya Ziwa (TAMASCA), Charles Chacha amesema;
"Elimu tuliyopata leo ni nzuri na itatusaidia sisi wakurugenzi wa
makampuni ya ulinzi binafsi kutenda kazi zetu za kila siku kwa kuelimisha
wajibu wa walimzi wetu namna ya utendaji wa kazi zao wanapokuwa lindoni."
"Tumekumbushwa
kuhakikisha tunafata taratibu zote za ajira hususan katika kuwalipa walinzi
mishahara kwa wakati kwa kufuata viwango vilivyowekwa na Serikali, kuwapa
mikataba ya kazi za ulinzi na kupeleka michango yao NSSF," ameongeza Bw.
Chacha.
0 Maoni