Waliokufa kwa kufunga wafikia 65, Ruto aamuru mhubiri ashtakiwe kwa ugaidi

 

Polisi nchini Kenya wanaendelea na operesheni kali ya kutafuta miili ya watu kwenye msitu ambao miili ya waumini  65 wa kanisa lenye mafunzo yenye utata imefukuliwa kwenye makaburi mafupi.

Kutokana na tukio hilo Rais wa Kenya William Ruto ameagiza kukamatwa haraka na kufunguliwa mashtaka kwa Mhubiri Paul Mackenzie ambaye aliwataka wafuasi wake kufunga hadi kufa ili waende mbinguni na kupelekea Waumini kupoteza maisha ambapo hadi sasa miili 65 imegunduliwa “Mackenzie ni Gaidi na atatakiwa kufungwa jela”.


Polisi wa Malindi wamesema zoezi hilo si la kutafuta miili tu bali pia kuwatafuta wafuasi ambao huenda bado wapo kwenye mfungo hadi kufa kama walivyoagizwa na mchungaji wao.


Uchunguzi wa kina unaendelea kwa kiongozi wa kanisa la Good News International Church aliyewaagiza waumini wake wafunge hadi kufa ili wakutane na Yesu Kristo.


Viongozi wa makanisa nchini Kenya wamelaani mafundisho hayo potofu ya Mchungaji Paul Mackenzie, yanayoenda kinyume na maandiko matakatifu.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya (IGP) Japhet Koome anatarajiwa kufika katika eneo la miili ilipofukuliwa hii leo.



Polisi nchini Kenya leo wamemkamata mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Mchungaji Zablon wa Yesu, akisoma Biblia katika eneo la gharama la hekari 800 linalomilikiwa na Mchungaji Paul Mackenzie, ambapo mtu huyo anadaiwa ni mshirika wa mtuhumiwa Mackenzie.



Chapisha Maoni

0 Maoni