Viongozi wa Dini, Wahariri wa Habari na Wadau mbalimbali wamebainisha sababu zinazochangia mmomonyoko wa maadili nchini na kuiasa jamii kurudi kwenye Maadili yanayozingatia Mila na Desturi.
Hayo yameelezwa
wakati wa kikao cha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Viongozi hao kwa lengo la
kujadili changamoto ya Mmomonyoko wa Maadili katika kikao hicho
kilichofanyika tarehe 24 Aprili, 2023 jijini Dar Es Salaam.
Wadau
hao wakijadili mada zilizowasilishwa kuhusu maadili, wamesema malezi
ya sasa yana changamoto kutokana na utandawazi, ukuaji wa teknolojia
na wazazi kushindwa kuwajibika.
Akizungumza kwa niaba ya
Jukwaa la Wahariri, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bakari Machumu
ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum kwa kutafuta suluhisho na kulichukulia suala la maadili kwa
uwazi ndani ya jamii.
"Kuwakutanisha Wahariri na vyanzo
vya taarifa na elimu ambao ni viongozi wa Dini na Wadau wengine
katika kikao hiki kitatupa fursa ya kwenda mbele zaidi kwani jukumu
letu kuhakikisha tunapohabarisha tunaufahamu na kitu hicho.
Umetujengea mahusiano na watoa taarifa" amesema Bakari
Machumu.
Kwa upande wake Mchungaji mstaafu na Mkurugenzi wa
Taasisi ya Hananja Compassion Foundation, Richard Hananja amesema
majadiliano hayo yamekuja kwa wakati muafaka kutafuta suluhisho la
changamoto ya maadili katika jamii.
"Watu wanakwenda
kwenye nyumba za Ibada, tutumie nyumba za ibada hasa kwa Waumini wa
Dini na Madhehebu mbalimbali kutoa elimu ya maadili kwa jamii"
amesema Mchungaji Hananja.
Naye Shekh Rashid Shemzigwa
aliyezungumza kwa niaba wa shekh wa mkoa wa Dar es Salaam, amesema
kuwe na muda wa kutosha wa kujadili masuala ya maadili kwa Wadau wote
Ili kuhakikisha changamoto ya mmomonyoko wa maadili inahubiriwa kila
mahali.
Akifungua kikao hicho Waziri wa Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amebainisha
kuwa lengo la kikao hicho ni kuhakikisha ajenda ya maadili
inamilikiwa na jamii yenyewe Ili kurudi kwenye utamaduni uliokuwepo
hapo awali.
"Mfano nenda kwenye mikutano ya jamii
ukauliza vipaumbele ni nini, utasikia afya, maji, elimu, umeme,
barabara, kilimo, mifugo na vitu kama hivyo, nadra sana kusikia
mmomonyoko wa maadili kuwa ni kipaumbele chetu. Bado umiliki wa hili
jambo tunatakiwa tuupeleke kwenye meza zote za maamuzi sekta zote"
amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Ameelezea Tamasha la kutangaza
fursa za kiuchumi kwa kushirikiana na Wadau litakalozinduliwa Aprili
27-29, 2023 mkoani hapa mwelekeo wake ni kumilikisha ajenda ya
maadili kwa wananchi na kuwaelimisha wananchi juu ya fursa za
kiuchumi. Aidha, amewashukuru Taasisi ya FAGDI kwa kujitoa kuandaa
tamasha hili pamoja na wadau wote waliochangia kuwezesha,
amewashukuru SMAUJATA na wengine wengi wanaoendelea kujitokeza
kuichukua ajenda hiyo.
Awali, akiwasilisha mada kwa
washiriki, Mtaalamu wa Saikolojia Dkt. Chris Mauki amewakumbusha
wazazi kutotumia muda mwingi kutafuta fedha Ili kuwarithisha watoto
wao badala ya kuwarithisha tabia njema yatakayosaidia kuwa na jamii
yenye maadili mema.
Na WMJJWM- Dar es Salaam
0 Maoni