Tume ya Madini imeendelea kuimarisha ukaguzi wa migodi
nchini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa lengo
la kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa usalama, ufanisi
na kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, hatua inayolenga kuhakikisha
rasilimali za madini zinanufaisha kizazi cha sasa na
kijacho.
Akizungumza Juni 19, 2026, katika Maonesho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park
jijini Dodoma, Afisa Mkaguzi wa Migodi wa Tume ya Madini, Rose Mika,
amesema ukaguzi wa mara kwa mara unaofanyika katika migodi mikubwa,
ya kati na midogo unalenga kuhakikisha shughuli za uchimbaji
zinaendeshwa kwa kuzingatia Sheria ya Madini pamoja na Kanuni za
Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za mwaka 2010.
Amesema
ukaguzi huo husaidia kubaini mapema changamoto zinazoweza kuhatarisha
usalama wa wafanyakazi na wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya
migodi, hivyo kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kabla ya kutokea
kwa madhara.
Rose amesema Tume ya Madini pia inaendelea
kusimamia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa mazingira, ikiwemo
kudhibiti uchafuzi wa maji, hewa na ardhi pamoja na kuhakikisha taka
zinazotokana na shughuli za uchimbaji zinahifadhiwa na kushughulikiwa
kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Aidha, amesema Tume
inafuatilia utekelezaji wa mipango ya kufunga migodi (Mine Closure
Plans) ili kuhakikisha maeneo yaliyokwishafanyiwa uchimbaji
yanarejeshwa katika hali salama na yenye tija baada ya shughuli hizo
kukamilika.
Kwa mujibu wa Rose, hatua hiyo ni muhimu katika
kuhakikisha ukuaji wa sekta ya madini unaenda sambamba na uhifadhi wa
mazingira na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Mbali
na ukaguzi wa migodi, Tume ya Madini inaendelea kusimamia matumizi ya
baruti katika shughuli za uchimbaji, ikiwemo utengenezaji, uingizaji,
usafirishaji na biashara yake kwa mujibu wa sheria na kanuni
zilizopo.
Katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Tume ya
Madini inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu fursa
mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo na kuwahamasisha kushiriki
katika shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini
pamoja na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kwa kuzingatia
matakwa ya sheria, ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.


0 Maoni