Katika jamii ya
Kimaasai, maisha ya mwanaume hupitia hatua mbalimbali za kimila
zinazoonyesha ukuaji, Miongoni mwa hatua hizo muhimu ni kufanyiwa
sherehe inayojulikana kwa jina la Orkiteng le Sirit ikimaanisha ni
mwisho wa ujana na kuingia uzeeni.
Katika hatua hii ambapo mtu
anatawazwa kuingia rika la uzee, wazee wa jamii hiyo huchagua Dume la
rika ambalo lina afya njema na lililohasiwa tangu utoto wake, dume
hili siku ya shughuli ndio hutolewa mwanzo kwenye boma lenye Ng’ombe
wengi na kumwagiwa maziwa kisha hunyongwa hadi kufa.
Sherehe
ya Orkiteng le Sirit , si sherehe ya kawaida bali ni tukio la heshima
kubwa linalofanyika kwa kufuata mila na desturi za kale
zilizorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kwa jamii ya Kimaasai, ni
hatua ya ukamilifu wa mwanaume na uthibitisho kwamba ametimiza
majukumu yake ya kifamilia na kijamii, kufanyiwa sherehe hii
hakuangalii umri ila inazingatia jinsia kwa kuwa anayefanyiwa sherehe
hii ni mwanaume pekee, vigezo vinavyoangaliwa ili mwanaume afanyiwe
sherehe hii, ni lazima awe ameoa, awe na watoto wa kike na kiume na
awe mtu mwema na maadili katika jamii.
Akizungumza wakati wa
sherehe hiyo, Alaigwanani wa kabila la kimasai Maningo Rinjo amesema
viongozi wa mila wa ukoo kama (Laizer, Mollel, Laitayo, Ngidong’i)
ndio wenye jukumu la kumchagua dume atakayechinjwa baada ya
kujiridhisha kuwa ana sifa zote zinazotakiwa kwa mujibu wa mila na
desturi za Kimaasai ili kutekeleza jukumu hilo la kijamii ambalo
linahudhuriwa na ndugu wote wa familia na jamii yote ya wamasai
inayozunguka Kijiji hicho.
“Si kila dume anaruhusiwa
kutumika katika sherehe hii, sisi viongozi wa mila hukagua na
kuthibitisha sifa zake kabla ya kutoa ruhusa ya kuchinjwa, dume wa
kutekeleza sherehe hii lazima awe amehasiwa tangu utotoni, hajawahi
kumpanda dume jike, pembe zake ziwe zimenyooka bila kupinda mithili
ya pembe za mbogo, asiwe mgonjwa na sifa zingine za ndani ambazo
viongozi wa kimila ndio huzichunguza kwa undani,” alisema
Alaigwanani Maningo Rinjo.
Alaigwanani Olonyori Lemoyan kutoka
Ukoo wa Laizer Kata ya Nainokanoka Ngorongoro alisisitiza kuwa si
kila mwanaume anastahili kufanya sherehe ya Orkiteng le Sirit, moja
wa masharti muhimu ili mwanaume afanyiwe tukio hilo kuwa
na
familia yenye watoto wa kike na kiume, awe na mali na uelekeo wa
maisha, mtu anayejali watu na awe ni rafiki wa ukoo wake na jamii
inayomzunguka pamoja na kupata ridhaa ya ukoo wake kufanya sherehe
hiyo.
“Orkiteng le Sirit ni heshima kubwa katika jamii ya
Kimaasai. Mwanaume lazima awe ametimiza wajibu wake wa kifamilia kwa
kupata watoto wa kike na wa kiume. Bila kutimiza sharti hilo, hawezi
kufikia hatua hii muhimu ya maisha,” alisema Alaigwanani Olonyori
Lemoyan.
Wakati wa sherehe hizo baada ya dume kunyongwa na
kutolewa nyama zake, mwanaume anayehitimu (anayepandishwa rika)
pamoja na mke wake na mama yake mzazi wanatakiwa hukalia utumbo wa
dume hilo kama ishara ya kuaga rasmi ujana na kuingia katika hatua ya
uzee. Kitendo hicho hubeba maana kubwa ya kiutamaduni na kuashiria
mwanzo wa jukumu jipya ndani ya jamii na kuachana na usharobaro na
mambo yote ya ujana.
Baada ya taratibu hizo kukamilika, rika
la Korianga huungana na mwenzao aliyeingia hatua ya uzee timilifu
huimba nyimbo za furaha na heshima huku wakielekea bomani,
wakimpongeza mwenzao kwa kufikia hatua hiyo adhimu. Nyimbo hizo
huashiria kukubalika kwake rasmi katika kundi la wazee na kupewa
nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mila, desturi na maamuzi
yanayohusu ustawi wa jamii.
Orkiteng le Sirit si tu sherehe ya
kuchinja dume laa hasha, ni alama ya mafanikio ya maisha, uwajibikaji
wa kifamilia na heshima ya kuwa mzee katika jamii ya Kimaasai. Hatua
hii ni urithi wa kipekee unaoendelea kuunganisha vizazi na kuhifadhi
utamaduni wenye thamani kubwa kwa jamii hiyo.



0 Maoni