Misime: Polisi Wafuatilia Wanaohamasisha Uhalifu Mitandaoni

 

MSEMAJI wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari kutokana na ushirikiano mkubwa linaoupata Jeshi la Polisi kutoka kwa wananchi pamoja na wadau wengine katika kubaini, kuzuia na kutanzua vitendo vya uhalifu.

Misime amesema pamoja na hali hiyo ya usalama kuwa nzuri, yapo matukio machache ya kihalifu yaliyojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini na ambayo yameendelea kushughulikiwa kwa ufanisi mkubwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi wamekuwa wakitoa taarifa mara kwa mara kuhusu kukamatwa kwa wahalifu waliotenda uhalifu, kufikishwa kwao mahakamani, na kwa baadhi yao kupatikana na hatia na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.

Misime amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na maswali kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu namna Jeshi la Polisi linavyofuatilia na kushughulikia vitendo vya uhamasishaji wa uvunjifu wa amani vinavyoonekana kufanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema Jeshi la Polisi linafuatilia kwa karibu sana shughuli zote za aina hiyo zinazofanywa na baadhi ya watu ambao awali walikuwa wakihamasishana kufanya maandamano nchini Julai 7.

Kwa mujibu wa Misime, kutokana na ufuatiliaji unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa saa 24 kupitia mifumo mbalimbali pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, imebainika kuwa watu hao wameondoka kwenye ajenda ya kuhamasisha maandamano yasiyozingatia matakwa ya sheria na sasa wanahamasishana kufanya vitendo vya uhalifu.

Amesema miongoni mwa vitendo hivyo ni kuhamasisha kufunga barabara, uchomaji moto wa shule ili kusababisha taharuki kwa wazazi na walezi, kushambulia wananchi, kukata watu vichwa na kuua baadhi ya watu, pamoja na kuharibu mali za umma na binafsi.

Misime amesema watu hao pia wamekwenda mbali zaidi kwa kuhamasishana kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii kuvamia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kuwapora silaha ili kuzitumia kufanya uhalifu wanaoupanga.

Amesisitiza kuwa uhamasishaji wa uhalifu huo wa kijinai unaofanywa chini ya kivuli wanachokiita haki ya kufanya maandamano ya amani haukubaliki kwa sababu ni kinyume na sheria za nchi, misingi ya utawala wa sheria pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa na ni hatari kwa usalama wa nchi.

Misime amesema hakuna haki ya kuhamasisha kufanya vitendo vya kihalifu vinavyokusudia kuhatarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao na vinavyokiuka haki za watu wengine kwa kuwajengea hofu kila siku na kutaka kuwanyima uhuru wao wa kufanya shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato.

Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na linaendelea kuwafuatilia kwa karibu sana kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana katika kukataa na kupinga vitendo vyote vya kihalifu vinavyolenga kuhatarisha maisha ya wananchi, mali zao, mali za umma na amani ya nchi.

Pia ameshauri mtu yeyote anayepokea ujumbe unaohamasisha uhalifu wa aina hiyo kutousambaza, bali kuufuta na kutoa taarifa kwa vyombo husika ili kuchukua hatua.

Misime amesema Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini itaendelea kuwa shwari, yenye amani, utulivu na usalama kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.



Chapisha Maoni

0 Maoni