Tanzania Yaweka Mkazo Ushirikiano na Africa50 Kukuza Miundombinu

 

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na Taasisi ya Africa50 pamoja na wanahisa wengine ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu barani Afrika. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders' Meeting-GSM) uliohitimishwa jana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo. 

Mhe. Balozi Omar, alieleza kuwa Tanzania, kama mwanahisa wa Africa50, inaiona taasisi hiyo kuwa chombo muhimu kinachounganisha Serikali, wawekezaji na taasisi za kifedha ili kubadilisha vipaumbele vya miundombinu kuwa miradi inayotekelezeka na yenye mvuto wa uwekezaji. 

Aliongeza kuwa Tanzania, kama mwanahisa wa Africa50, inaiona taasisi hiyo kuwa chombo muhimu kinachounganisha Serikali, wawekezaji na taasisi za kifedha ili kubadilisha vipaumbele vya miundombinu kuwa miradi inayotekelezeka na yenye mvuto wa uwekezaji. 

"Maono ya Africa50 yanaendana kikamilifu na dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050 (Dira 2050), inayolenga kuifikisha nchi katika uchumi wa kipato cha juu cha kati na kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050" alisema Mhe. Balozi Omar. 

Aidha, aliwakaribisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na kwingineko, akieleza kuwa Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu unaoadhimisha miaka kumi ya mafanikio ya Africa50 tangu kuanza kwa shughuli zake. 

"Tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu hapa Dar es Salaam, Tunatumaini mtapata majadiliano yenye tija pamoja na kufurahia ukarimu wa Tanzania," alisema Mhe. Balozi Omar. 

Alisisitiza kuwa Miundombinu ni msingi wa kufikia azma hiyo, hususan katika sekta za nishati, usafirishaji na mifumo ya usafirishaji wa bidhaa, ambayo ni muhimu katika kukuza uzalishaji, biashara na uchumi kwa ujumla. 

Mhe. Balozi Omar aliongeza kuwa Tanzania iko tayari kuendelea kushirikiana na Africa50 pamoja na wanahisa wengine katika kuvutia uwekezaji endelevu, kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati na kuimarisha uunganishwaji wa kikanda kwa manufaa ya wananchi wa Afrika. 

"Nawashukuru washiriki wote kwa michango yenu yenye kujenga, na maamuzi yaliyofikiwa hapa yataisaidia Africa50 kuimarisha nafasi yake katika muongo ujao wa maendeleo ya miundombinu barani Afrika" alisema Mhe. Balozi Omar. 

Mkutano huo umezikutanisha nchi wanahisa, taasisi za kifedha na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa lengo la kujadili namna bora ya kuendeleza na kufadhili miradi ya miundombinu barani Afrika.

Chapisha Maoni

0 Maoni