Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Zainab
Katimba, amewataka wakuu wa Idara na Vitengo vya Sheria katika Tawala za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanazingatia weledi, uadilifu, na
uwajibikaji katika majukumu yao ili kuepusha uzembe unaoigharimu serikali.
Akizungumza
Februari 12, 2025 kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe.
Mohamed Mchengerwa, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili cha wakuu
wa idara hizo jijini Dodoma, Mhe. Katimba amesema kuna uzembe wa hali ya juu
katika usimamizi wa mashauri ya madai.
"Katika
baadhi ya maeneo, mashauri ya madai yameendeshwa upande mmoja kwa zaidi ya
miaka mitano na maamuzi kufikiwa dhidi ya serikali bila mwanasheria wa
halmashauri husika kuhudhuria hata mara moja mahakamani," amesema.
Ameongeza
kuwa serikali haiwezi kuvumilia uzembe huu, hasa pale ambapo halmashauri
hulazimika kulipa mabilioni ya shilingi baada ya kushindwa kesi kwa sababu ya
kutohudhuria mahakamani au kusimamia vibaya mashauri.
Mhe. Katimba
pia amebainisha changamoto katika usimamizi wa mikataba, ambapo baadhi ya
mikataba hufikia ukomo bila mamlaka husika kuchukua hatua mapema za kuongeza
muda wake, hali inayosababisha utekelezaji wa majukumu nje ya utaratibu wa
kisheria.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wakili Richard
Odongo, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujadili changamoto hizi na kuweka
mikakati madhubuti ya kuongeza uwajibikaji na uadilifu katika sekta ya sheria
ndani ya halmashauri.
0 Maoni