Wakuu wa Vyombo vya Habari na Wahariri Waandamizi
waandamizi wa Tanzania wametoa Azimio la pamoja lenye nguvu wakisisitiza
umuhimu wa kulinda amani na kukemea vikali kauli za uchochezi zilizosikika hivi
karibuni nchini.
Aidha Wakuu hao wa Vyombo vya Habari na Wahariri
Waandamizi walitangaza kuungana na viongozi wa dini na makundi mengine katika
kusisitiza umuhimu wa kutunza amani kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29
Oktoba.
Azimio hilo, lililotolewa leo, Oktoba 25 linatoa
tahadhari kubwa kuhusu athari za “Uwendawazimu wa Kihalaiki” unaoweza
kulisambaratisha Taifa.
Katika Azimio hilo, viongozi hao wa vyombo vya
habari wamewataka Watanzania kukataa kuhudhuria karamu ya uchochezi wenye lengo
la kuwashawishi kulewa "Uwendawazimu wa Kihalaiki".
Aidha walieleza kuwa mataifa mengi yaliyotumbukia
katika machafuko, ikiwemo Rwanda, Kongo, Sudan, na majirani wengine, yamebaki
na makovu ya kihistoria kutokana na aina hiyo ya machafuko.
Wamesisitiza kuwa machafuko, mateso na mauaji ya
raia yaliyotokea katika nchi hizo yalichangiwa na ubinafsi wa vikundi vya
wanasiasa walioamua kutumia propaganda za kugawanya watu bila kujali maslahi
mapana ya mataifa yao.
Azimio hilo lilikemea moja kwa moja kauli za hivi
karibuni nchini Tanzania, ambazo zimeelezwa kuwa zinazochochea chuki na shari
na haziakisi kabisa utamaduni wa Mtanzania. Viongozi hao wa vyombo vya habari
walionya kuwa kauli zinazohamasisha wananchi kufanya vurugu, kuchoma vituo vya
mafuta, vituo vya polisi na mali nyingine, siyo tu ni kosa kisheria, bali ni
kauli zisizoakisi Utanzania na zinazopaswa kukemewa na kila Mtanzania.
Mataifa yanayoingia katika machafuko huanza na kauli
chochezi za mtu mmoja mmoja, kisha vikundi, na hatimaye hutengeneza
"Uwendawazimu wa Kihalaiki" kupitia vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii.
Azimio linakumbusha kwamba Tanzania ilipata uhuru
kupitia jitihada za majadiliano na hoja, ambapo wanasiasa walipingana bila
kupigana. Kutokana na misingi hii, nchi imebaki kuwa kisiwa cha amani na makazi
ya matumaini kwa wakimbizi wanaokimbia vita katika nchi zao.







0 Maoni