Tanzania inazidi kuimarisha mkakati wake wa
kihistoria wa kujitosheleza kwa sukari, ikilenga kufuta kabisa utegemezi wa
bidhaa hiyo muhimu kutoka nje ya nchi.
Mafanikio haya yamepigwa jeki na kuanza uzalishaji
kwa viwanda vipya vinavyoahidi kukidhi mahitaji ya jumla ya Taifa yanayofikia
tani 807,000 kwa mwaka.
Huku Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ukikaribia,
Serikali na wadau wa maendeleo wanasisitiza kuwa, kura ya kila Mtanzania ndiyo
ngao pekee ya kulinda na kuendeleza kasi hii ya uchumi wa viwanda.
Kwa sasa, mahitaji ya sukari nchini yamegawanyika
katika matumizi ya kaya yanayofikia takribani tani 552,000 na mahitaji ya
viwandani yanayokadiriwa kufikia tani 255,000.
Uzalishaji wa ndani umekuwa ukikabiliwa na pengo,
hasa kwenye sukari ya viwandani, ambapo Taifa limekuwa likiagiza kiasi kikubwa
cha zaidi ya tani 250,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, ili kukabiliana na changamoto hii,
Serikali imekaza buti kwa kuunganisha nguvu za viwanda vikuu vinne (Kagera,
Mtibwa, Kilombero na TPC) na uwekezaji mkubwa katika viwanda vipya.
Jitihada za upanuzi na uwekezaji zimeleta matunda.
Kiwanda cha Sukari Mkulazi II kimekamilika na kimeanza uzalishaji, kikiongeza
uwezo wa Taifa kwa tani 50,000 kwa mwaka.
Kiwanda hiki kinamilikiwa kwa ubia na Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza, na ni mfano wa uwekezaji wa Taifa
katika kujiletea maendeleo.
Vilevile, Kiwanda cha Sukari Bagamoyo kimeanza
kuchangia sokoni, kikitoa wastani wa tani 17,000 kwa mwaka.
Mafanikio haya yanaongezewa nguvu na ujenzi wa
Kiwanda cha Sukari Kasulu, ambacho kinatarajiwa kuwa mhimili muhimu katika
kufikia lengo la uzalishaji kamili wa kitaifa.
Lengo la Serikali kupitia viwanda hivi vipya na
upanuzi wa vingine ni kufikia jumla ya uzalishaji wa tani 655,000 kwa mwaka
mara vitakapokamilika, huku dhamira kuu ikiwa ni kuondoa kabisa uagizaji wa
sukari ifikapo mwaka 2025, na kuanza kusafirisha nje ya nchi.
KAMPENI YA KURA: LINDA UWEKEZAJI HUU!
Mafanikio haya ya kiuchumi hayana budi kulindwa kwa
nguvu ya kidemokrasia. Kampeni za uchaguzi zinahimiza Watanzania kutambua kuwa
kura ndio dhamana yao ya kuendelea kwa kasi hii.
Kura yako inachagua viongozi watakaohakikisha
uwekezaji huu mkubwa katika Mkulazi II unalindwa na kuendelezwa.
Aidha, kura yako inamchagua Rais na Wabunge
watakaoweka sera endelevu za kulinda viwanda vya ndani na kuwasaidia wakulima
wa miwa, badala ya kuruhusu uagizaji usiodhibitiwa.
Zaidi ya
yote, kujitokeza kwako kupiga kura kwa amani ndio udhibitisho mkuu wa utulivu
wa kisiasa unaohitajika kuendeleza ujenzi wa viwanda vingine kama kile cha
Kasulu.
Inahimizwa kila Mtanzania ajitokeze kwa wingi na kwa
utulivu siku ya uchaguzi. Kura yako ndiyo sauti ya maendeleo, na ndiyo muhuri
utakaofunga kabisa pengo hili la sukari na kutufanya Tanzania kuendelea
kuimarika kuwa Taifa la Viwanda!

0 Maoni