Wananchi
wa kata ya Masama Magharibi, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wameishukuru
Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Jiweni–Masama
yenye urefu wa Km 16 kwa kiwango cha changarawe, ambayo imeleta unafuu mkubwa
wa kiuchumi na kijamii.
Bi.
Emiliana Natai, mkazi wa kijiji cha Lukani, amesema barabara hiyo ilikuwa
chanzo cha usumbufu mkubwa kwa wakazi, hasa nyakati za mvua ambapo wanafunzi
walichelewa shuleni na wengine kushindwa kupata chakula kwa wakati.
“Wakazi
wa Jiweni, Mashua na Munguamawe waliteseka sana, nyakati za mvua, barabara
ilikuwa haipitiki kabisa lakini sasa kila mtu anafurahia maendeleo haya,
tunaishukuru Serikali”, amesema Emiliana.
Ameongeza
kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumewawezesha wakulima kusafirisha mazao yao
kwa urahisi hadi sokoni, hatua iliyochochea ongezeko la kipato kwa mtu mmoja
mmoja na kuongeza mapato ya taifa kupitia biashara vijijini.
Kwa
mujibu wa Bw. Liviston Mushi, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amesema wananchi
walilazimika kubeba mizigo kichwani au kuwalipa vibarua kwa gharama kubwa
kuwasaidia kuvusha bidhaa zao kwenda sokoni.
“Kwa muda
mrefu tulitegemea kubeba mazao yetu vichwani, tena kwa tabu kubwa lakini sasa
masika yote yamepita barabara ikiwa salama. Ni hatua kubwa ya maendeleo tunayopaswa
kuishukuru,” amesema Mushi.
Naye, Bw.
Musa Kirundwa amesema kabla ya mradi huo walilazimika kuajiri vijana wa nguvu
kwa malipo ya juu ili waweze kuwasaidia kusafirisha bidhaa sokoni, jambo ambalo
lilikuwa mzigo mkubwa kiuchumi.
“Barabara
hii ni ya muhimu sana kiuchumi kwa sababu pia inapita watalii wanaopanda Mlima
Kilimanjaro ikiwekewa kiwango cha lami, itavutia watalii wengi zaidi na kuinua
uchumi wa eneo hili,” amesema Kirundwa.
Afisa
Mtendaji wa kijiji cha Lukani, Suzani Lyiamboko amesema barabara hiyo imekuwa
mkombozi mkubwa kwa wafanyabiashara ambao sasa wanafikia masoko kwa urahisi
tofauti na awali ambapo walikumbwa na adha ya usafiri.
“Tunaishukuru
TARURA kwa kazi nzuri waliyoifanya, barabara hii sasa inapitika mwaka mzima na
wananchi wanaweza kusafirisha mazao yao bila hofu ya mvua wala tope,” amesema Lyiamboko.
Hata
hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo kwa kuacha
kutupa taka kwenye mifereji ya maji ili isizibe na kuharibu barabara wakati wa
mvua kwani barabara hiyo ni muhimu kwa wakazi wa Hai, na wilaya jirani ya Siha.
Kwa
upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Hai, Mhandisi Kuya Francis amesema
ujenzi wa barabara hiyo upo chini ya mradi wa RISE unaogharamiwa na mkopo nafuu
toka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha
miundombinu ya barabara vijijini kwa lengo la kufungua fursa za kijamii,
kiuchumi na kuimarisha huduma kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.



0 Maoni