Katika tukio adimu,
lenye uzito wa kitaifa na la kihistoria, Jamii ya Kimaasai nchini Tanzania
imeonyesha heshima ya hali ya juu kwa Katiba na Demokrasia kwa kuahirisha zoezi
lao muhimu la kimila la tohara ili kuhakikisha vijana zaidi ya 1,000
wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huu uliotolewa
na Laigwanani Mkuu, Isack Ole Kisongo Meijo, si tu tamko la uzalendo, bali ni
pigo zito kwa wale wote wanaopanga njama za vurugu, maandamano, au mbinu za
kuvuruga amani na mfumo wa kikatiba wakati au baada ya uchaguzi.
Darasa la Uzalendo
kwa Taifa
Kwa kuahirisha tukio
hilo kuu la kimila, ambalo kwa kawaida huathiri uwezo wa vijana wengi kushiriki
kupiga kura, Maasai wameweka kiwango kipya cha kuheshimu mfumo wa kidemokrasia.
Laigwanani Ole
Kisongo alisisitiza wazi kuwa amani, uwajibikaji wa kiraia, na kura ni
kipaumbele kinachozidi hata matukio makuu ya utamaduni wao.
"Jamii ya
Kimaasai imeonesha mfano wa kuigwa. Huu ndio uzalendo tunaoutaka. Kura ndiyo
sauti ya maendeleo, na amani ndiyo msingi wa taifa letu," alikariri Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, akipongeza hatua hiyo.
Pigo kwa Wapanga
Vurugu
Kitendo hiki cha
Maasai kimepokelewa kama ishara ya wazi kwamba Watanzania wanajua wanachotaka:
Wanaamini katika mabadiliko ya kimaendeleo yanayofuata Katiba na yanayotawaliwa
na amani na utulivu.
Uamuzi wa Waasai
kuahirisha mila yao kwa ajili ya kupiga kura unatoa ujumbe mkali na wa moja kwa
moja kwa wale wanaopanga mbinu za kuingia madarakani au kuleta mabadiliko
kupitia njia za vurugu au maandamano yasiyo halali: Watanzania wamechagua
sanduku la kura, siyo vurugu.
Kabla ya sherehe kuu
za tohara, Maasai wameweka neno la mwisho: Wanaheshimu mfumo wa kidemokrasia na
Katiba.
Ikiwa kabila lenye
utamaduni tajiri linaamini kwenye kura, maana yake ni kwamba njia ya amani ndiyo
njia pekee ya mabadiliko inayokubalika na Watanzania walio wengi.
Waasai wanawaonyesha
Watanzania wote njia: Kura Kwanza, Vurugu Haikubaliki. Hii inathibitisha kuwa
utashi wa Taifa ni kuona maendeleo ya nchi yanaendelea katika mazingira ya
utulivu na uwajibikaji wa kikatiba.

0 Maoni