Wakati Taifa likielekea katika kipindi cha Uchaguzi,
mjadala mkali umeibuka kuhusu njia bora ya kufikia mabadiliko ya kisiasa, huku
baadhi ya wachambuzi wakihimiza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kujifunza kutoka kwa kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Hayati Raila
Odinga.
Kiini cha mjadala huo, mtandaoni ni kauli
iliyozungumzwa na mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kimataifa na siasa ndugu
Majid Mjengwa wakati akihojiwa na mmoja ya vyombo vya habari nchini.
Ilielezwa na Majid kuwa mshauri huyo wa karibu wa
Chadema, ameonesha kwamba uvumilivu na kufuata utaratibu ndio suluhishi la
mizozo na huonesha ukomavu wa kisiasa, na kwamba mazungumzo ndiyo yanayoleta
mabadiliko na si vurugu.
Washiriki waliochangia katika mtandao wengi wao
walisisitiza umuhimu wa Chadema kutanguliza majadiliano, wakimtumia Odinga kama
mfano wa kiongozi aliyekuwa karibu na upinzani wa Tanzania na ambaye, kulingana
na wao, alishika falsafa ya majadiliano katika siasa.
Hata hivyo, mijadala ya mtandaoni inaonyesha maoni
yaliyogawanyika kuhusu rekodi ya Odinga na mbinu anazopaswa Chadema kuiga.
Baadhi wanaeleza kuwa licha ya Odinga kuwa mshauri, historia yake ya kisiasa
pia inajumuisha matukio ya kususia Uchaguzi na kujiapisha kama 'Rais wa
wananchi' baada ya Mahakama Kuu kuamuru Uchaguzi urudiwe, hatua iliyofuatiwa na
vurugu na maafa. Wanaona matukio haya kama mifano ya kuepukwa, wakisisitiza
kuwa kususia Uchaguzi si suluhisho.
Mjadala pia uliibua hoja kuhusu msimamo wa Odinga
mwenyewe, akitajwa kuwa alihimiza Wakenya kuandamana. Wengine wanahoji iwapo,
baada ya matukio hayo, Odinga mwenyewe alishika Nchi.
Licha ya utata huo, jumbe nyingi zinaweka mkazo
katika wito wa ukomavu. Mchambuzi mmoja anahoji kuwa hali ya kukosekana kwa
mazungumzo kati ya Chadema na watawala imekuwa changamoto, ingawa anakiri
kwamba suala la siasa za Afrika na historia ya viongozi wake (kama vile Odinga
kuhukumiwa kwa uhaini na kisha kukubali mazungumzo kwa maslahi ya Taifa) ni
elimu tosha.
Mwisho wa yote, jumbe hizo zinahitimisha kwa ujumbe
mmoja mkuu, kama inavyoelezwa: "Demokrasia mahala ambapo hakuna uvumilivu
haiwezi kuota mizizi." Ujumbe huu unasisitiza haja ya viongozi na wafuasi
wa kisiasa kukumbatia uvumilivu, kufuata taratibu za kikatiba na Sheria, na
kutanguliza mazungumzo kama njia kuu ya kutatua migogoro na kuleta mageuzi
nchini.

0 Maoni