Hospitali
ya Benjamin Mkapa (BMH) inatarajia kuanzisha huduma mpya ya kumuondolea mama
mja mzito maumivu wakati akijifungua kupitia njia ya huduma ya usingizi na
ganzi salama kitaalamu inaitwa Epidural anaesthesia.
Hayo
yamesemwa na Mtaalamu wa matibabu ya usingizi na ganzi salama wa BMH Fredrick
John wakati akitoa mafunzo kwa Watumishi wa Afya na Elimu kwa Wateja wa BMH
kama sehemu ya kuadhimisha siku ya usingizi na ganzi salama Duniani.
"Imeonekana
baadhi ya wanawake wajawazito wanaogopa yale maumivu ya uchungu wakati wa
kujifungua hivyo wanaomba kujifungua kwa upasuaji, sasa huduma hii
tunayoianzisha itamuwezesha mama mja mzito ajifungue kwa njia ya kawaida bila kusikia maumivu na
sio kujifungua kwa upasuaji," alielezea Fredrick.
Huduma
hiyo itatolewa kwa ushirikiano wa Wataalamu wa usingizi na ganzi salama,
Madaktari wa Magonjwa ya wakina mama na Wauguzi Wakunga na kuwa tayari
maandalizi ya vifaa, wataalamu na miongozo viko kwenye hatua nzuri na huduma
itaanza kutolewa mwezi Januari 2026.
Nae Mkuu
wa Idara ya huduma za usingizi na ganzi salama Dkt. John Venancy Misago amesema
kuwa huduma hiyo itakwenda sambamba na kuanzisha matibabu ya maumivu kwa
kutumia utaalamu wa usingizi na ganzi salama badala ya dawa ya vidonge vya
maumivu (Intervention Pain Management).
"Matibabu
hayo ya kitaalamu yatasaidia Wagonjwa wenye Maumivu ya muda mrefu, wenye
magonjwa mengine kama ya kansa na wanapata maumivu na Wagonjwa waliotibiwa kwa
kufanyiwa upasuaji," aliongezea Dkt. Misago.
Ameongezea
kuwa idara yake itatoa mafunzo kwa watoa huduma wa BMH na kisha itaanza
programu ya kuzijengea uwezo hospitali nyingine na kuanzisha timu ya Wataalamu
wa kuwafuatilia Wagonjwa wa maumivu.
Kaimu
Mkurugenzi wa BMH Dkt. Henry Humba pamoja na kuwapongeza Wataalamu hao wa
usingizi na ganzi amewataka wasiishie hapo bali kujiendeleza kwa ngazi za juu
zaidi kwa kutambua Hospitali ya Benjamin Mkapa inaendelea kukua,
inaendelea kubuni na kuwekeza huduma mpya nyingi ambazo zitahitaji kutumia.
Na. Jeremia Mwakyoma
Picha: Na. Jeremia Mbwambo


0 Maoni