TMDA yashikilia tena hadhi ya juu ya udhibiti wa dawa Afrika - WHO

 

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kuthibitishwa kwa mara nyingine kuwa imefanikiwa kushikilia hadhi ya Kiwango cha Tatu cha Ukomavu (WHO Maturity Level 3) wa mfumo wa udhibiti wa dawa na chanjo, hatua inayodhihirisha uimara wa mifumo ya afya nchini.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA imeeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na tathmini ya kina iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2023, ambayo imethibitisha kuwa TMDA inaendesha shughuli zake kwa uwazi, weledi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyolenga kulinda afya ya jamii.

“TMDA inajivunia hatua hii ya mafanikio kwa kuwa inadhihirisha umahiri wa kazi za udhibiti kwa uwazi, weledi na kwa kufuata viwango vinavyokubalika kimataifa katika kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za afya,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mwaka 2018, Tanzania iliweka historia kwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupitia TMDA kufikia kiwango hiki cha tatu cha WHO (ML3), hatua iliyotambuliwa kimataifa kama kigezo muhimu cha kuaminika katika udhibiti wa dawa na chanjo.

Kuthibitishwa tena mwaka 2023 baada ya ukaguzi wa kina uliofanywa na WHO ni ushahidi kuwa TMDA si tu ilifikia viwango hivyo, bali pia imeendeleza mifumo bora ya udhibiti ambayo ni endelevu na thabiti.

Aidha, TMDA inasema mafanikio haya yanafungua fursa mpya kwa Tanzania kushiriki kwenye programu za pamoja za udhibiti wa dawa na vifaa tiba, kuongeza ushiriki kwenye masoko ya kikanda na kimataifa, na pia kuimarisha mvuto kwa wawekezaji kwenye sekta ya afya.

TMDA imewaalika Watanzania wote kusherehekea mafanikio haya kama nchi, na kutoa shukrani kwa wadau mbalimbali waliotoa mchango wao katika safari hii ya mafanikio.

Kwa mafanikio haya, Tanzania inaendelea kujijengea hadhi ya kuwa kinara wa mifumo ya udhibiti wa afya Afrika, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuhakikisha ustawi na ulinzi wa afya ya wananchi wake.




Chapisha Maoni

0 Maoni