MGOMBEA
Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, leo Oktoba 17, 2025, amehitimisha kampeni zake
katika Mkoa wa Dodoma, ambapo maelfu ya wananchi walijitokeza kumsikiliza
akiwasilisha sera na ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Katika
ziara yake ya kampeni mkoani humo, Dk. Nchimbi amefanya mikutano mikubwa katika
wilaya za Mpwapwa, Kongwa, Kondoa na Dodoma Mjini, akisisitiza dhamira ya CCM
kuendeleza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za afya,
elimu, kilimo, maji na miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara na reli ya
kisasa (SGR) kutoka Dodoma–Kigoma na Dodoma–Mwanza, endapo wananchi watakipatia
chama hicho ridhaa ya kuendelea kuongoza kwa miaka mitano ijayo.
Amesema,
Serikali ya CCM pia imepanga kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Msalato, pamoja na ujenzi wa uwanja mkubwa wa mpira wa miguu jijini Dodoma,
ambao utatumika kwa mashindano ya AFCON 2027, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya
kukuza michezo na utalii wa kimataifa.
Dk.
Nchimbi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia
Suluhu Hassan, kwa kuimarisha chama hicho na kukipa heshima ndani na nje ya
nchi kupitia uongozi wake wenye hekima, uwazi na mageuzi ya kiuchumi.
Aidha,
alimpongeza kwa ujasiri wa kuendeleza utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati
iliyoanzishwa na Hayati Dk. John Pombe Magufuli, ikiwemo ujenzi wa reli ya
kisasa (SGR), bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, na kuhamishia makao makuu ya
nchi Dodoma.
Akiwa
anahitimisha kampeni mkoani humo, Dk. Nchimbi amewahimiza wananchi wa Dodoma na
Watanzania kwa ujumla kumpigia kura za ushindi wa kishindo Mgombea Urais wa
CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wabunge na madiwani wa chama hicho,
akisisitiza kuwa “ushindi wa CCM ni uhakika wa kuendeleza mafanikio ya
maendeleo yaliyopatikana.”
Kufikia
Mkoa wa Dodoma, Balozi Dk. Nchimbi anakuwa amefanya kampeni katika mikoa 24
tangu kuzinduliwa rasmi kwa kampeni hizo Agosti 28, 2025, jijini Dar es Salaam,
akipita kila pembe ya nchi kuomba kura kwa ajili ya Dk. Samia Suluhu Hassan,
wabunge na madiwani wa CCM.



0 Maoni