WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi
kwa makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za
kiuchumi na kijamii.
Amesema
Serikali inafanya hivyo kwa kutambua kuwa kundi la Wajasiriamali ni muhimu na
nguzo katika katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia shughuli zao.
Amesema
hayo leo Ijumaa (Oktoba 17, 2025) wakati wa mkutano wake na makundi mbalimbali
ya Wajasiriamali wa jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla iliyofanyika kwenye
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini humo.
“Ninyi no
watu muhimu sana kwenye uchumi wa nchi hii, na mmetoa mchango mkubwa sana
kwenye uchumi wa nchi hii, nataka niwahakikishie Serikali hii inanufaika nawe
na ndio maana Serikali inaendelea kuwathamini na inapanga mipango mbalimbali
juu yenu, Endeleeni kuimarisha biashara zenu, hatutawatupa mkono.”
Amesema
kuwa katika kuhakikisha kundi hilo linanifaika, Serikali ya awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza programu mbalimbali
zenye lengo la kuwawezesha Wajasiriamali nchini ikiwemo Utekelezaji wa programu
zakuwezesha wananchi kupata mitaji, Masoko na mafunzo ya ujasiriamali.
Programu
nyingine ni Programu ya Taifa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, kusimamia
uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo kupitia programu za uwezeshaji
wajasiriamali, Uendelezaji wa kongani za wajasiriamali pamoja na kutenga maeneo
katika kila Halmashauri kwa ajili ya shughuli za kilimo, viwanda, biashara na
shughuli nyingine muhimu za kiuchumi.
Katika
hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa Serikali itaendelea msukumo wa kuhamasisha
na kusimamia uanzishwaji na usajili wa vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika na
makampuni, pamoja na kuwawezesha kupata mitaji na elimu ya matumizi ya mitaji
hiyo ili waweze kuendesha shughuli zao kwa uhakika.
“Viongozi
kwenye halmashauri, fuatilieni mienendo ya biashara za Wajasiriamali katika
maeneo yenu, ikiwa kuna changamoto zitatueni, lengo ni kuona kama tunapata
ufanisi au la, lazima tujue wanafanikiwa kwa kiasi gani.”
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaanzisha programu maalumu za kuwawezesha
vijana waliomaliza taasisi za elimu ya juu na kati kuingia katika ajira na
kujiajiri. “Programu hizi zitahakikisha vijana wanapata mitaji, elimu ya
ujasiriamali, ardhi, na mazingira wezeshi ili kushiriki kikamilifu katika
shughuli wanazokusudia”.
Naye,
waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy
Gwajima amesema kuwa anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kusimamia maono yake ya
kuhakikisha kuwa ananyanyua kundi la Wajasiriamali ili yaende safari ndefu ya
kumiliki uchumi wa Tanzania.
Wakizungumza
katika mkutano huo, viongozi wa Wajasiriamali hao wameishukuru Serikali ya
awamu ya Sita kwa jitihada mbalimbali ambazo imekuwa ikizifanya katika
kuhakikisha kundi hilo linaendelea kustawi na kusaidia katika kukuza uchumi wa
mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.




0 Maoni