Benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Tanzania imechangia kiasi cha Shilingi milioni 20 kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea hundi kutoka benki hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema benki hiyo imetumia falsafa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na upendo na kuleta matumaini kwa watoto wenye uhitaji wa matibabu ya moyo.
"KCB wamefanya tendo jema la upendo kwa kuwapa watoto wenye magonjwa ya moyo matumaini na kuleta faraja katika familia zinazopitia changamoto ya kuuguza watoto hao kwa muda mrefu", alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema changamoto kubwa inayoongeza idadi ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini ni pamoja na wazazi kutokuwa na uelewa kuhusu magonjwa hayo hivyo kuishi maisha yanayoweza sababisha magonjwa ya moyo ikiwemo kula lishe duni hasa wakati wa ujauzito, unywaji wa pombe uliokithiri, matumizi ya sigara, na wakati mwingine magonjwa hayo husababishwa na vina saba.
"Asilimia kubwa ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanatoka katika falimia zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu, Serikali yetu imekuwa mstari wa mbele kuwasaidi watoto wenye magonjwa hayo kwa asilimia 70 na asilimia 30 iliyobaki inatolewa na Taasisi pamoja na wadau mbalimbali", alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliongezea kuwa JKCI ni Taasisi pekee yenye uwezo wa kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 400 ndani ya mwaka mmoja katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati, na kuainisha kuwa gharama za matibabu hayo ugharimu kati ya shilingi milioni 8 hadi shilingi milioni 20 kwa mtoto mmoja.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Vihatarishi na Uzingatiaji kutoka Benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Tanzania Angelina Semioni alisema KCB imepata fursa ya kugusa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
"Leo KCB imekabidhi msaada wa shilingi milioni 20 kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo kwa kugharamia matibabu pamoja na kuhakikisha watoto hao wanapata matibabu endelevu", alisema Angelina.
Angelina alisema KCB inaungana na jamii katika kusaidia matibabu kwani wanaamini kuwa kila mtoto anastahili fursa ya kuishi hivyo wakaona waweze kuwezesha uwezo wa kifedha utakaowezesha kuokoa maisha.
"Kwetu sisi mchango huu una maana kubwa kuliko thamani ya fedha tunayoitoa, kila mtoto atakayefanyiwa upasuaji tunaamini atakuwa na mafanikio makubwa na tutaweza kupata maendeleo endelevu kama taifa kupitia watoto hawa tunaowasidia leo", alisema Angelina.
Nao wazazi wa watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa na Taasisi hiyo wamewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kuchangia gharama za matibabu ili kuwezesha watoto wao kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Anna Gaspari mzazi wa mtoto mwenye magonjwa ya moyo alisema baada ya kufika katika Taasisi hiyo na mtoto wake kufanyiwa uchunguzi na kutakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo alipewa gharama za shilingi milioni 10 ambazo hakuwa na uwezo wa kulipia.
"Sikuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu ili mwanangu aweze kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha valvu za moyo lakini kupitia kitengo cha ustawi wa jamii mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo kupitia fedha zinazotolewa na wadau kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto", alisema Anna.

.jpeg)
0 Maoni