ZAIDI ya wananchi 300 wametembelea banda la Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) tangu kuanza kwa Maonesho ya
Wiki ya Utumishi wa Umma, wakipata elimu na ufafanuzi kuhusu
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara za wilaya katika maeneo
yao.
Hatua hiyo imeendelea kuimarisha uhusiano kati ya
wananchi na taasisi hiyo, huku ikitoa fursa ya kusikiliza na kutatua
changamoto zinazowakabili wananchi moja kwa moja.
Akizungumza
katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa
Umma Bi. Catherine Sungura amesema wananchi wanaowasilisha kero zao
huunganishwa moja kwa moja na mameneja wa maeneo husika ili kupata
maelezo ya kina na ufumbuzi wa haraka.
“Tunawapokea wananchi
wengi kutoka maeneo tofauti ya Tanzania ambao wengi wanataka kufahamu
ujenzi au matengenezo ya barabara katika maeneo yao na hivyo wengi
wao wanapata majibu hapo hapo kwani wanazungumza moja kwa moja na
mameneja wa mkoa au wilaya husika”.
Amesema lengo la TARURA
ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi
inayotekelezwa pamoja na hatua mbalimbali za maendeleo yake.
Bi.
Sungura ametolea mfano wa mwananchi mmoja kutoka Kimara jijini Dar es
Salam Bi. Sarah James Joseph ambaye amefika katika banda na kutaka
kujua ujenzi wa barabara ya Kimara mwisho hadi king’ongo ujenzi
wake umefikia wapi ambapo mwananchi huyo ameweza kuwasiliana na
Meneja wa Wilaya ya Ubungo na kupata ufafanuzi na hivyo kupokea
majibu kwa furaha na kuridhika na huduma aliyoipata kwenye banda la
TARURA.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa barabara ya
King'ongo iliyopo Kimara, Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Bi.
Sungura amesema barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha zege kuanzia
TRA kuelekea King'ong'o ambapo kilomita 1.6 pekee zimebaki na kati ya
hizo, mita 800 zinatarajiwa kujengwa kuanzia Julai mwaka huu, huku
sehemu iliyobaki ikikamilishwa katika awamu inayofuata.
Bi.
Sungura amesisitiza kuwa TARURA itaendelea kuboresha miundombinu ya
barabara ili kurahisisha usafiri na mawasiliano kwa wananchi na
kwamba barabara bora huchochea upatikanaji wa huduma za kijamii,
biashara na shughuli nyingine za maendeleo, hatua inayochangia kuinua
ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa maeneo mbalimbali nchini.
Kwa
upande wake Bi. Sarah James Joseph mkazi wa King'ongo, Kimara jijini
Dar es Salaam ameishukuru TARURA kwa kazi zao na juhudi kubwa
wanazozifanya kila siku kwaajili ya kuwasaidia wananchi katika
suala la mawasiliano ya barabara nchini.



0 Maoni