Na. Mwandishi Wetu
Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa onyo kali kwa wananchi
wanaofuata mkumbo wa kushawishiwa kuvunja sheria na amani ya taifa,
akisisitiza kuwa serikali haitavumilia mtu au kikundi chochote
kinacholenga kuichoma moto nchi kwa maslahi binafsi.
Akizungumza
kwa masikitiko makubwa na waumini wa Msikiti wa Mukadam uliopo Kata
ya Chang’ombe, Wilaya ya Dodoma Mjini wakati wa mashindano ya
Qur’an na harambee ya ujenzi wa msikiti huo, Katambi alisema kuwa
amani na umoja wa nchi ndio misingi mikuu ya maendeleo ambayo
haipaswi kuchezewa hata kidogo.
Waziri Katambi alifafanua kuwa
katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la kauli za
uchochezi na kibaguzi zinazolenga kudhoofisha Muungano na kuleta
mifarakano kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kisiasa, jambo
ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi na ustawi wa jamii.
Kuhusu
mipango ya siri na wazi ya baadhi ya watu wanaoandaa na kuhamasisha
maandamano haramu yanayopangwa kufanyika Julai 7, 2026, Katambi
alipiga marufuku vitendo hivyo na kubainisha kuwa hatua hizo zisizo
za kisheria zina lengo la kuingiza taifa kwenye machafuko, hivyo
amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kukataa katakata kushawishiwa
au kutumiwa kama chambo cha kuvunja sheria.
Aliwakumbusha
wananchi kuwa kuishi kwa kufuata mikumbo ya kisiasa bila kutafakari
madhara yake kunaweza kubomoa taifa kwa sekunde chache, wakati ujenzi
wa amani iliyopo umegharimu miaka mingi ya jasho na uzalendo wa hali
ya juu.
Waziri Katambi alihitimisha kwa kutoa agizo madhubuti
kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kote kuendelea kuchukua hatua
kali na za haraka bila muhali kwa yeyote atakayebainika kujihusisha
na uchochezi, huku akitoa rai kwa kila Mtanzania kuheshimu maelekezo
ya mamlaka ili kudumisha utulivu na maendeleo ya kiuchumi.

0 Maoni