Mwanahabari Mkongwe na
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Dk Samwilu Mwafisi, ametoa mwito
kwa wanahabari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuzingatia
uandishi wenye kulinda maslahi ya taifa, huku akionya dhidi ya
kufuata mikumbo inayoweza kuchochea uvunjifu wa amani na kuichoma
nchi moto.
Akizungumzia wajibu wa tasnia hiyo, Dk Mwafisi
alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuunda mtazamo wa
jamii, ambapo vinaweza kujenga au kubomoa taswira ya nchi, hivyo
uzalendo na maadili yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya
kukimbilia faida za kifedha au umaarufu wa muda mfupi.
Alibainisha
kuwa mabadiliko ya TEHAMA yameleta changamoto ya watu kusambaza
habari potofu na za kusisimua bila uhakiki, jambo linalotumiwa na
watu wenye nia ovu kushawishi jamii kufuata mikumbo ya kuvunja
sheria, hususan wakati wa migogoro ambapo maslahi na usalama wa taifa
lazima vipewe kipaumbele ili kulinda wananchi.
Dk Mwafisi
alihitimisha kwa kusitiza kauli yake ya kutoficha changamoto bali
kusema ukweli kwa weledi, akitoa rai kwa kila mwenye simu, kamera na
kalamu kutoitumia kama silaha ya kujichafua au kuhatarisha amani,
bali kuwa daraja thabiti la maendeleo na mshikamano kwa maslahi
mapana ya nchi.

0 Maoni