Wakimbizi wapatao
155,811 wanaohifadhiwa katika maeneo mbalimbali nchini wameiomba
Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na
wananchi wote kuendelea kulinda amani iliyopo, wakibainisha kuwa
kukosekana kwa amani kunasababisha watu kupoteza kila kitu na
kulazimika kukimbilia nchi nyingine na kwamba yaliyowakuta wao ni
mfano hai.
Wakimbizi hao wametoa kauli hiyo jijini Dar es
Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, ambayo
huadhimishwa kila mwaka mwezi Juni, yakiwa na kaulimbiu isemayo “Hadi
Kila Mtu Awe Salama”.
Walitoa shukrani za dhati kwa Rais
Samia Suluhu Hassan, na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kuwapa
hifadhi na usalama bila ubaguzi.
Akizungumza katika
maadhimisho hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi,
amesema Tanzania inapaswa kujifunza kutokana na hali zilizotokea
katika nchi jirani na kuendelea kuimarisha mazingira ya amani na
utulivu.
Amesema serikali itaendelea kuwahudumia wakimbizi
waliopo nchini na kuhakikisha usalama wao, huku akisisitiza kuwa
amani ni msingi muhimu unaowezesha wananchi kujikita katika shughuli
za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.
Alieleza kuwa ni agizo
la Rais Samia kuwa serikali itaendelea kuwahudumia wakimbizi wote
waliopo nchini kwa kuzingatia utu na haki za binadamu.
Alikumbusha
kuwa msimamo wa Tanzania kwa sasa ni kuhimiza urejeaji wa hiari wa
wakimbizi kwenda maeneo salama kama suluhisho bora zaidi.

0 Maoni