Banda la Tume ya Madini limeendelea kuwa kivutio
kikubwa kwa mamia ya wananchi wanaotembelea Maonesho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park
jijini Dodoma, huku wengi wakijitokeza kupata elimu kuhusu sekta ya
madini, huduma zinazotolewa na Tume pamoja na fursa zilizopo katika
shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini.
Miongoni
mwa waliotembelea banda hilo ni Lusajo Luena kutoka Dodoma, ambaye
amesema elimu aliyoipata imemwezesha kuelewa taratibu za upatikanaji
wa leseni za madini na wajibu wa wamiliki wa leseni katika kuendeleza
maeneo yao ya uchimbaji.
"Kabla ya kufika hapa sikuwa na
uelewa wa kina kuhusu namna leseni za madini zinavyotolewa na
kusimamiwa. Leo nimepata elimu ya kutosha kuhusu taratibu mbalimbali
na umuhimu wa kuzingatia sheria za madini," amesema Luena.
Kwa
upande wake, Joyce Kitundu kutoka Dodoma amesema maelezo aliyopata
katika banda hilo yamemsaidia kufahamu mchango mkubwa wa sekta ya
madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa na namna Serikali
inavyosimamia rasilimali za madini kwa manufaa ya
wananchi.
"Nimejifunza kuwa sekta ya madini ni nguzo
muhimu ya maendeleo ya nchi. Pia nimeelewa majukumu ya Tume ya Madini
katika kusimamia shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini,"
amesema Kitundu.
Naye Glory Daudi kutoka Kondoa amesema elimu
aliyopata imefungua fursa mpya za uelewa kuhusu ushiriki wa vijana na
wanawake katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya
madini.
"Nimefurahishwa na elimu niliyopewa kuhusu fursa
zilizopo kwenye sekta ya madini. Sasa nimeelewa kuwa si lazima mtu
awe mchimbaji pekee, kwani kuna fursa nyingi za biashara na utoaji
huduma zinazozunguka sekta hii," amesema Daudi.
Tume ya
Madini inaendelea kutumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma kuhusu
majukumu yake, huduma mbalimbali zinazotolewa pamoja na kuhamasisha
ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya
madini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

.jpeg)

0 Maoni