Tembo ni
mnyama wa aina gani?! Je mnyama huyu ana faida gani katika sayari hii
tuliyomo?! Kwanini Tanzania inajivunia kuwa na tembo?! Kwanini
mikataba ya kimataifa inamlinda tembo?!! Kwanini tembo, kwanini?
Nauliza kwanini ?!!
Haya ni maswali, maswali yanayosumbua
fikra za binadamu, ambapo Kwa wengi wetu tukimtazama tembo,
tunamwona ni mnyama mkubwa mwenye nguvu nyingi, anayepita porini
aking'oa miti na wakati mwingine kuingia mashambani kusababisha
uharibifu na hata kuleta madhara kwa binadamu. Lakini kuna swali
ambalo wengi wetu hatujawahi kujiuliza, kwamba Je, nyuma ya ukubwa
wake huo, athari zake kuna kazi gani kubwa anayoifanya kwa manufaa ya
viumbe wengine na hata binadamu?
Ukweli ni kwamba tembo si
mnyama wa kawaida. Ni mnyama mwenye maajabu mengi ambayo watafiti
walitumia miongo kadha wa kadha kuvumbua . Hivi umewahi kujua kuwa
tembo ni mhandishi kwa asili yake?!! Naam, tembo ni mhandisi wa
mazingira ambaye kazi zake zinawezesha maisha ya maelfu ya viumbe
kuendelea kuwepo kila siku katika sayari ya dunia.
Fikiria
msitu mkubwa uliokauka wakati wa kiangazi. Mito imepungukiwa maji,
mabwawa yamekauka na viumbe wengi wako katika hatari ya kufa kwa kiu.
Katika mazingira hayo magumu, anaibuka mnyama tembo ambaye kwa
kutumia meno na miguu yake anachimba maeneo yenye unyevunyevu hadi
maji yatoke ardhini. Anapomaliza kunywa na kuondoka, swala,
pundamilia, nyani, ndege na viumbe wengine wengi huja kutumia maji
hayo. Bila kujua, tembo huwa ameokoa maisha ya mamia ya viumbe ambao
hawana uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Si hivyo tu. Tembo
anapotembea mamia ya kilomita kutafuta chakula, hubeba mbegu za miti
mingi kupitia kinyesi chake na kuzisambaza maeneo mbalimbali. Mbegu
hizo huota na kuwa miti mipya. Miaka inapopita, miti hiyo hugeuka
kuwa misitu inayovutia mvua, kuhifadhi maji na kutoa hewa safi
tunayovuta kila siku. Kwa lugha rahisi, tembo ni mpandaji miti wa
asili ambaye hafanyi kampeni wala kutafuta sifa wala kutambuliwa,
lakini matokeo ya kazi yake yanaonekana kwa vizazi vingi.
Katika
misitu minene, tembo amekuwa akifungua njia kwa kuvunja matawi na
kusafisha mapito. Njia hizo hutumiwa na wanyama wengine kutafuta
chakula, maji na maeneo salama ya kuishi. Hata mbegu zinazoota
ardhini hupata nafasi ya kukua kwa sababu mwanga wa jua hupenya
kwenye maeneo aliyopita. Hivyo, tembo si mnufaika wa mazingira pekee;
bali ni mmoja wa watengenezaji wakuu wa mazingira hayo.
Jambo
ambalo wengi hatulioni ni kwamba faida za tembo hazibaki porini tu.
Maelfu ya watalii kutoka duniani kote huja Tanzania kushuhudia uzuri
wake. Wageni hao huacha fedha zinazochangia uchumi wa Taifa, kuongeza
ajira kwa vijana na kusaidia ukuaji wa biashara mbalimbali katika
jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi. Kwa namna hiyo, tembo anageuka
kuwa daraja linalounganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya
wananchi.
Sasa, hebu tufikirie kwa undani zaidi. Kama tembo
wote wangetoweka leo, nani angechimba visima vya asili wakati wa
ukame? Nani angesambaza mbegu za maelfu ya miti kwa umbali mkubwa
kiasi hicho? Nani angeendelea kufungua njia za asili zinazotumiwa na
viumbe wengine porini? Ukweli ni kwamba baadhi ya kazi anazozifanya
tembo haziwezi kufanywa kwa ufanisi uleule na mnyama mwingine
yeyote.
Ndiyo maana tunapomtazama tembo, tusione ukubwa wake
pekee wala tusikumbuke madhara yake pekee. Tumuone kama mhandisi wa
mazingira/ikolojia, mzalishaji wa misitu, mtoa maji kwa viumbe
wengine na mshirika muhimu wa maisha duniani. Kadiri tunavyozidi
kumwelewa, ndivyo tutakavyogundua kuwa tembo si mzigo wa mazingira,
bali ni moja ya zawadi kubwa ambazo asili imeikabidhi Tanzania, na
Mungu ameitunuku dunia kwa ujumla wake
Endelea kubaki katika
kurasa za TAWA ujifunze mengi kuhusu wanyamapori na faida zao kwetu.
Tchao!!
📞 +255 676 475 541

0 Maoni