Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia S. Hassan
anatarajiwa kufungua rasmi Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji
Tanzania (TMIC 2026) utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026 katika
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es
Salaam.
Akizungumza leo Juni 27, 2026 wakati wa uzinduzi wa
TMIC 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema serikali
imeamua kujenga uchumi wa viwanda unaotokana na madini kwa kuwekeza
katika uchakataji na uyeyushaji wa madini badala ya kuendelea kuuza
malighafi.
Amesema kaulimbiu ya mkutano huo, "Madini
Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi,"
inaakisi dira ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha
uchakataji wa madini barani Afrika.
Kwa mujibu wa Mhe.
Mavunde, amesema Tanzania tayari ina viwanda vinane vya kusafisha
dhahabu, huku Mkoa wa Dodoma ukiwa na viwanda tisa vinavyojengwa na
vinavyoendelea na uzalishaji pamoja na kiwanda kikubwa cha kuyeyusha
madini ya nikeli na shaba.
"Zaidi ya Sh bilioni 600
zinawekezwa katika ujenzi wa kiwanda cha chuma kitakachotumia
asilimia 100 ya malighafi za ndani, huku uwekezaji mwingine
ukiendelea Kigamboni na Tanga kwa ajili ya uchakataji wa madini ya
'Heavy Mineral Sands' na mradi wa madini ya niobium wa Panda Hill,
Mbeya," amesema Mhe. Mavunde
Amesema, katika kuongeza
ushiriki wa Watanzania kwenye sekta hiyo, thamani ya manunuzi
kupitia mpango wa 'Local Content' imefikia Sh trilioni 5.1, huku
bidhaa 20 zikitakiwa kuzalishwa na wazawa kwa ajili ya kuhudumia
migodi mikubwa.
Amesisitiza wafanyabiashara kuzingatia
uaminifu na viwango vya kimataifa ili kunufaika zaidi na fursa
hizo.
Amesema sekta ya madini imeendelea kuimarisha mchango
wake katika uchumi kwa kuingiza Sh trilioni 1.374 katika Mfuko Mkuu
wa Serikali, kiwango kilichovuka lengo la Sh trilioni 1.2 kwa mwaka
huu wa fedha.
Mhe. Mavunde, amesema Serikali imeidhinisha
asilimia 10 ya mapato yote ya sekta ya madini kuelekezwa kwenye
utafiti wa kina wa jiofizikia ili kuongeza maeneo yanayofahamika kuwa
na madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka
2030.
Aidha, amesema Serikali inaandaa mfuko maalumu wa mikopo
kwa wachimbaji wadogo, ambao licha ya changamoto za mitaji na
teknolojia, wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya
madini.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaanza
operesheni ya kufuta kidijitali leseni zote za madini zisizotumika.
Wamiliki watakaoshindwa kuwasilisha taarifa ndani ya muda uliowekwa
watapewa notisi ya siku 30 kabla ya leseni hizo kujifuta moja kwa
moja.
Nae, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya
Samamba, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha utajiri wa madini
unakuwa chachu ya kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na
kuimarisha uchumi kupitia uongezaji thamani badala ya kuishia kwenye
uchimbaji pekee.
Amesema TMIC 2026 utawakutanisha viongozi wa
Serikali, taasisi za fedha, kampuni za madini, wataalamu wa
teknolojia, watafiti na wadau wengine kutoka duniani kote kujadili
fursa za uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.
"Huu ni
wakati wa kuingia katika awamu mpya ya uwekezaji, ubunifu na ukuaji
wa sekta ya madini nchini," amesema.
Kwa upande wa Katibu
Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka,
amesema mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya
2,000 na watoa mada zaidi ya 100 kutoka mataifa zaidi ya 50, huku
zaidi ya mada 20 zikijadiliwa zikiwemo sera, kodi, uwekezaji,
teknolojia, nishati safi, madini ya kimkakati, uongezaji thamani na
masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG).
Mchwampaka
amesema TMIC 2026 pia utaweka mkazo katika maendeleo ya wachimbaji
wadogo pamoja na ushirikishwaji wa wanawake na watu wenye ulemavu
katika mnyororo mzima wa uongezaji thamani wa madini. Mkutano huo
unatarajiwa kufungwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.



0 Maoni