Waangalizi
wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wametakiwa kuzingatia sheria za nchi na
kuepuka kuingilia au kushiriki katika vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri au
kuingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba
2025 wakati wanapotekeleza majukumu yao ya uangalizi.
Wito huo
umetolewa leo tarehe 17 Oktoba 2025 na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, wakati akifungua kikao cha
siku moja na Waangalizi hao kwa lengo la kuwapa maelekezo, taarifa muhimu na
miongozo kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao ya uangalizi wa uchaguzi kwa
mujibu wa sheria.
Katika
hotuba yake, Mhe. Jaji Asina amewakumbusha waangalizi hao kutekeleza majukumu
yao kwa uadilifu, uhuru, na kutokuwa na upendeleo, huku wakizingatia sheria za
nchi na Mwongozo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa mwaka 2025.
“Waangalizi
wanapaswa kuepuka kuingilia shughuli za uchaguzi, kutoonyesha dhihaka kwa
watendaji wa uchaguzi, au kutoa maelekezo kwa maafisa wa Tume kuhusu namna ya
kufanya kazi zao,” amesisitiza Jaji Asina.
Mhe Jaji
Asina ameongeza kuwa endapo kuna malalamiko au dosari yoyote inayojitokeza,
waangalizi hao hawana budi kuwasilisha malalamiko hayo kwa Tume Huru ya Taifa
ya Uchaguzi kwa njia ya Tume.
Katika
kikao hicho, mada tatu kuu ziliwasilishwa kwa waangalizi wa uchaguzi ambapo
mada ya Maandalizi ya Uchaguzi iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi mada ya
ma Masuala ya Usalama iliwasilishwa na mwakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania,
na mada kuhusu Masuala ya Afya iliwasilishwa na mwakilishi kutoka Wizara ya
Afya.
Pia
Waangalizi hao walikabidhiwa nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha
kutekeleza majukumu yao. Nyaraka hizo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani Na. 1 ya 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya 2024,
Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2025, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa 2025 na
Mwongozo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa 2025.
Aidha,
walikabidhiwa vitambulisho rasmi na kuaswa kuvitumia wakati wote wa kutekeleza
majukumu yao. Pia walihimizwa kujitambulisha kwa Wasimamizi wa Uchaguzi katika
maeneo watakayofika ili kurahisisha ushirikiano na kupata msaada inapohitajika.


0 Maoni