Serikali
ya Awamu ya Sita imefanikiwa kutangaza nyongeza ya Kima cha chini cha Mshahara
kwa sekta binafsikwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka Shilingi 275,060/= hadi
358,322/= ambapo kitaanza kutumika rasmi ifikapo 1 Januari, 2026 hatua
inayolenga kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua maslahi ya wafanyakazi nchini.
Akitangaza
amri hiyo, leo (17 Oktoba 2025) Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na
waandishi wa habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Ridhiwan Kikwete alisema mchakato wa upangaji wa Kima kipya cha
chini cha mshahara umekamilika na kwamba umezingatia mamlaka aliyopewa chini ya
Kifungu cha 39 (1) cha Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura 300.
“Kwa
mujibu wa Amri hiyo, Sekta za Kima cha chini cha Mshahara zimeongezeka kutoka
13 za mwaka 2022 hadi 16 kwa mwaka 2025 na kutoka sekta ndogo 25 za mwaka 2022
hadi 46 kwa mwaka 2025. Kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kwa wastani wa
asilimia 33.4 kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/= na kitaanza kutumika
rasmi tarehe 1 Januari, 2026”, alisema Waziri Ridhiwani Kikwete.
Kwa
mujibu wa Waziri Ridhiwani , Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara imegusa sekta
za kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na
viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya
baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma
nyinginezo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara kwa Sekta
Binafsi Dkt. Suleiman Rashid Mohamed alisema mchakato wa majadiliano ulikuwa
shirikishi ambapo vyama vya wafanyakazi, waajili na waajiliwa vilishiriki
kikamilifu katika hatua zote.
Naye
Naibu Katibu Mkuu Shirikishio la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Rehema
Ludanga alisema kitendo cha Serikali kutangaza amri ya kupanda kwa mishahara
kwa kima cha chini cha sekta binafsi ni faraja kwa wafanyakazi nchini kwani
kimeonesha dhahili namna Serikali inavyothamini maslahi ya wafanyakazi nchini.
Rehema
aliongeza kusema ni wakati sasa waajili wote katika sekta binafsi kutekeleza
amri hiyo kwa kupandisha mishaharana
ikibidi zaidi ya kiwango kilichotangazwa ili kuongeza maslahi bora ya
wafanyakazi wao .
Suzanne
Ndomba-Doran Afisa Mtendaji Mkuu Chama cha Waajili Tanzania (ATE) akizungumza
kwenye kikao hicho alisema Chama kilishiriki kikamilifu kwenye mchakato kupitia
kamati ya wataalam ambapo maoni yote yaliyokusanywa toka mikoa yote nchini na
yamefanyiwa kazi hatua inayotoa urahisi wa utekelezaji wa amri hiyo..
Aidha,
Mtendaji Mkuu huyo aliwasihi waajili kutumia muda huu kabla ya kufika tarehe 01
Januari 2026 kufanya mazungumzo yatakayopelekea kubadilisha ulipaji wa
mishahara kwa mujibu wa amri iliyotangazwa na Serikali na kwamba ATE itaendelea
kutoa elimu na taarifa kwa waajili wote nchini kutekeleza amri hii.
Na. OWM - KVAU


0 Maoni