Mawakala wa Milki nchini wametakiwa kujisajili katika mfumo wa Wizara ya Ardhi ili kuingia kwenye mfumo rasmi utakaowezesha kutambulika.
Hayo
yameelezwa jana tarehe 12 Februari 2025 na Mratibu wa Mjadala kuhusu Utambuzi
na Usajili wa Wadau wa Sekta ya Milki Bi. Nuru Kimbe, mjadala uliofanyika
mkoani Arusha.
Amesema, ni
vizuri mawakala wa milki wakajisajili katika mfumo ili waweze kutambulika
katika kipindi hiki ambacho wizara inategemea kuwa na sheria ya milki.
"Nasisitiza
mawakala waweze kujisajili na waweke ‘details’ za masingi kama anuani na mahali
wanapofanyia kazi,"amesema Bi. Nuru.
Kwa mujibu wa
Bi. Kimbe ambaye ni Afisa kutoka Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, faida za kujisajili ni pamoja na kutambulika na serikali
kitu alichokieleza kitarahisisha kazi kwa mawakala ambapo amesema hatua hiyo
itarahisisha katika kazi zao kama wakala na kuwafikia wateja sambamba na kuaminika
zaidi.
Amebainisha
kuwa, kwa sasa mijadala inafanyika kwenye majiji ambako soko la milki
linafanyika sana na kuitaja majiji hayo kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha
na Mwanza.
Hata hivyo,
amesema wako katika mchakato wa kufika mikoa mingine inayokuwa sana katika soko
la milki kama vile Tanga, Morogoro, Pwani na Mbeya huku nia ikiwa ni kufika
nchi nzima.
Kwa upande
wake mmoja wa washiriki wa kikao hicho kutoka kampuni ya GimcoAfrika Ltd Bw.
Herien Muro amesema, elimu waliyopata kupitia kikao kazj ni muhimu kwa kuwa
inaenda kuondoa udanganyifu huku ikiisaidia serikali kupata mapato.
Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia kitengo cha Milki (REAL
ESTATE) inaendesha mijadala ya pamoja na
wadau kwa lengo la kupata maoni kuhusu utambuzi na usajili wa wadau wa sekta ya
milki ili kuboresha na kukuza sekta ya milki nchini.
0 Maoni