Serikali
kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA) imeendelea
kuhamasisha wawekezaji mbalimbali duniani kushiriki katika Duru ya Tano ya
Kunadi Vitalu vya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika Bahari Kuu ya Hindi
na Nchi Kavu itakayozinduliwa mwezi Machi mwaka huu.
Matangazo ya
fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia yanaendelea kupitia
Kongamano na Maonesho ya Wiki ya Nishati ya India yanayofanyika katika Jiji la
New Delhi, India tukio ambalo linawashirikisha zaidi ya watu 70,000 kutoka nchi
zaidi ya 50 Duniani.
Katika Banda
la Tanzania kwenye Maonesho hayo washiriki wengi wamevutiwa na taarifa za
kijiofizikia zinazobainisha utajiri wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia
zilizopo Tanzania.
Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye anashiriki Kongamano
hilo, ametembelea banda hilo la Tanzania na kuipongeza PURA kwa kutumia
majukwaa ya kitaifa na kimataifa kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya
Mafuta na Gesi Asilia.
Dkt. Biteko
ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha vyanzo vyake vyote vya nishati
vinaendelezwa ili kuwa na uhakika wa
nishati ya kutosha wakati wote.
Katika
kuelekea kwenye duru hiyo ya Tano ya Kunadi Vitalu vya utafutaji wa mafuta na
gesi asilia, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema PURA
imekamilisha masuala mbalimbali ikiwemo kupata Kampuni ya Kijiofizikia iitwayo TGS ASA yenye utaalam wa kuchakata data za mafuta na
gesi asilia ambayo pia inahusika na utangazaji wa data hizo katika masoko
mbalimbali duniani .
Mhandisi
Sangweni amesema kampuni hiyo itatakiwa kukusanya na kuchakata data za mitetemo
katika maeneo mengine ya bahari kuu ambayo hayajafanyiwa kazi ili kuongeza
taarifa na data za petroli kwa wawekezaji.
Ameongeza
kuwa, PURA imeshakamilisha uandaaji wa ramani inayoonesha maeneo ambayo yatatangazwa
kwenye duru ya tano inayojumuisha vitalu 26
ambapo vitalu 23 viko kwenye kina
kirefu cha Bahari ya Hindi na vitalu vitatu vipo Ziwa Tanganyika.
Amesema Duru ya tano ya Kunadi vitalu vya utafutaji
wa mafuta na gesi asilia itafanyika mwezi Machi, 2025 katika Mkutano na Maonesho
ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Petroleum Conference
and Exhibitions (EAPCE’25) Jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo
yatakwenda pamoja na maonesho ya kitaalam kuhusu jiolojia ya mafuta na gesi
asilia ya Tanzania; wawekezaji kuangalia taarifa za kijiolojia, kununua zabuni,
kuwasilisha zabuni, kufanya tathmini ya zabuni zilizowasilishwa na kupokelewa,
kufanyika kwa majadiliano ya mikataba (PSAs), kupata idhini ya Serikali ya
kusaini PSAs kutoka Wizara ya Nishati na Baraza la Mawaziri na Kusaini Mikataba
kati ya Serikali na Wawekezaji wawatakaoshinda.
Ametaja faida
mbalimbali zitakazopatikana baada ya Serikali kunadi vitalu hivyo kuwa ni
kuongezeka kwa mapato ya kodi kwa Serikali, mirabaha na gawio la faida
itokanayo na rasilimali itakayogundulika, mauzo ya data na tozo za leseni
pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania na kazi kwa makampuni ya
kitanzania.
katika
Kongamano hilo linaloendelea nchini India, Dkt.Biteko alipata fursa ya
kutembelea na kuzungumza na Watendaji wa Wizara ya Umeme ya India pamoja na
Watendaji wa kampuni ya Shell ambayo ni moja ya wawekezaji katika mradi wa LNG
ambapo aliwaeleza Watendaji wa Shell kuwa Serikali inataka kuona majadiliano
yanakamilika na mradi unaanza kutekelezwa.
Dkt. Biteko
alifuatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini ambao ni Mhe. Juliana Masaburi, Mhe. Ussi Pondeza na Mhe. Iddi
Kassim Iddi.
0 Maoni