Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) ihakilishe inatoa kandarasi za ujenzi na ukarabati
wa barabara kwa wakandarasi wenye uwezo wa kujenga kwa viwango vinavyoendana na
thamani ya fedha.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 13, 2025) wakati
akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbasi Tarimba aliyehoji kwanini Serikali isianze kutumia
vikosi kazi vya Manispaa au TARURA badala ya wakandarasi binafsi katika ukarabati
wa barabara zilizoharibika, katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, bungeni
jijini Dodoma.
“Tunaitaka TARURA iwasimamie wakandarasi binafsi wanapopewa
kazi, wawe na uwezo wa kujenga barabara za kudumu kwa mujibu wa viwango
vilivyopo ili barabara ziweze kutumika kwa muda mrefu. ”
Amesema kuwa awali mfumo wa ujenzi wa barabara za vijijini
uliokuwa unaruhusu Halmashauri kukarabati barabara zake ulibaini kuwa na
mapungufu hasa kutokana na uwezo tofauti wa kifedha wa baadhi ya Halmashauri.
“Serikali iliwasikiliza waheshimiwa Wabunge ambao wakati
wote mlipokuwa mnaomba baadhi ya barabara zenu kwenye Halmashauri zihamishiwe
TANROADS, kutokana na maombi ya mara kwa mara tuliamua kuunda TARURA
inayoshughulikia barabara za vijijini na mijini na inafanya vizuri. ”
Kadhalika Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali
itaendelea kutoa fedha kwa TARURA kwa ajili ya matengenezo ya muda mfupi.
“TARURA tumieni fedha hii vizuri ili kufanya ukarabati kwenye barabara zenye
uhitaji wa kukarabatiwa ili ziendelee kutumika. ”
Wakati huohuo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali
inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya udhibiti wa ugonjwa wa Malaria
ikiwemo uendeshaji wa kampeni ya usafi ambayo inagusa pia maeneo yenye mazalia
ya mbu. “Pia tunaendelea na utoaji wa neti kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania
kujikinga na Malaria”.
Ameongeza kuwa
Serikali inaendelea kutoa hamasa kwa wawekezaji kujenga viwanda vya
kutengeneza dawa za kutibu ugonjwa malaria na za kupuliza jwenye mazalia ya
vijidudu vya Malaria.
“Wengi mnafahamu kuwa pale Kibaha mkoani Pwani tunacho kiwanda cha kutengeneza
dawa za kunyunyiza kwenye mazalia ya mbu, Halmashauri sasa zinapaswa kutenga
fedha ili kwenda kununua dawa na kunyunyiza kwenye maeneo yote yenye mazalia ya
mbu. ”
Akijibu Swali la Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum
aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwalinda na kujenga ushindani wa
wawekezaji wazawa, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imetengengeza
mazingira nafuu ya uwekezaji kwa wazawa kwa kupunguza kiwango cha uwekezaji
kutoka Dola laki moja hadi dola elfu hamsini.
“Tumeendelea pia kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji
biashara kwa wazawa ikiwemo kupunguza kiwango cha kodi kwa bidhaa
zinazozalishwa ndani na hata mchakato wa upataji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
”
0 Maoni