Rais Samia anaendelea kupeleka furaha na neema kwa watumishi wa umma Tanzania - Kikwete

 

Waziri Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini ili kuongeza ufanisi wa taasisi za umma na kuleta huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza katika mkutano wa maafisa tawala na maafisa rasilimali watu uliofanyika katika Ukumbi wa AICC mkoani Arusha, Mhe. Ridhiwani amesema amewakumbusha watumishi hao kutekeleza wajibu wao na kuleta furaha kwa watumishi wa umma ili nao waweze kupeleka furaha na neema kwa Watanzania. Amesema hatua hiyo inatokana na maamuzi mbalimbali yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini.

Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali kupandisha madaraja watumishi 219,042 ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha utumishi wa umma nchini. Hatua hiyo imepata ridhaa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Pia, amesema Serikali imeongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 mwaka 2025 pamoja na kuongeza kima cha chini katika sekta binafsi kwa asilimia 33.4 kwa mwaka 2025/26. Ameeleza kuwa maboresho hayo yatazigusa sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, baharini, madini na utamaduni.

Kwa mujibu wa Waziri Mhe. Ridhiwani Kikwete, matokeo ya kitakwimu yanaonyesha kasi ya mageuzi ya kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hali inayotafsiriwa kuwa ni uongozi wa kimkakati unaoweka mbele ustawi wa watumishi pamoja na kuongeza ufanisi wa taasisi za umma nchini.




Chapisha Maoni

0 Maoni