Waziri wa
Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amesisitiza vyombo
vya habari nchini kuendelea kuandaa vipindi vyenye tija pamoja na kutumia
matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Prof. Palamagamba Kabudi ametoa kauli hiyo leo Februari 13, 2025 katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji 2025 unaofanyika Jijini Dodoma, kuanzia Februari 13 -14, 2025.
Amesema kwamba lugha ya Kiswahili kwa Watanzania inakabiliwa na changamoto sana, “moja tumeanza kufubaza Kiswahili, Tanzania tumeanza kufubaza Kiswahili kwa kuyafanya maneno ya kawaida ya Kiswahili kuyapa maana isiyo sahihi na hivyo kuwafanya watu waache kuyatumia.”
“Pia,
tumekuwa tunadumaza lugha ya Kiswahili kwa maana ya kuwa legelege kwa kuacha
kutumia utajiri wa lugha ya Kiswahili kwa kurudia maneno yaleyale wakati lugha
ya Kiswahili inautajiri mkubwa zaidi wa istilahi,” amesema Prof. Kabudi.
Ameongeza
kuwa lakini kwa sasa tatizo ambalo limeanza kuwa sugu ni la kubananga lugha ya
Kiswahili, “tunaanza kusema uyu na sio huyu, uyo na sio huyo, apa na sio hapa, hana
badala ya ana.” “Kuna mtu aliwahi kuniletea ujumbe anashida akaniandikia hana,
nikamuambia kumbe unacho,” amesema Prof. Kabudi,
Amesema watu
wengi wanaozungumza lugha ya Kiswahili katika nchi zinazotuzunguka wamekuwa
wakisema Watanzania ni wazungumzaji wa Kiswahili lakini sio mahiri tena wa
Kiswahili fasaha na sanifu, “kwa hiyo tuache kubananga Kiswahili kufubaza
Kiswahili, tuache kudumaza Kiswahili na wabanangaji wakubwa wa Kiswahili ni
watangazaji wasio kuwa mahiri katika matumizi ya kugha kwa kutia mbwebwe na
haraka ambazo zinaishia kufubaza na kudumaza Kiswahili.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Kuwe Bakari amesema kwa sasa TCRA ipo katika hatua za mwisho ya kukusanya takwimu za utangazaji kwa ajili ya kuwa data za watanzazaji nchini.
“Takwimu hizi
ni muhimu ili kujua idadi halisi ya watangazaji katika kufanikisha TCRA kutoa
huduma zake kwa watangazaji wote kutokana na kuwa na data zao,” amesema Dk.
Jabiri.
Mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) unaofanyika Jijini Dodoma unakauli mbiu isemayo, “Wajibu
wa Vyombo vya Utangazaji Kuelekea Uchaguzi Mkuu”.
0 Maoni