Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia
kufanya ziara ya kikazi Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia kesho tarehe
15/02/2025 kushiriki Mkutano wa Kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika (AU).
Mkutano huo
unatarajia kuchagua Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025 ambaye
atachukua nafasi ya Mwenyekiti wa sasa wa nchi ya Jamhuri ya Kiislamu ya
Mauritania.
Taarifa
iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Sharifa Nyanga imesema
mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika
ikiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna sita.
Vilevile,
mkutano utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye mkutano wa nchi
tajiri duniani (G20) utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Taarifa
ya kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Mbali na
masuala hayo, mkutano pia utajadili ajenda ya kuhusu matumizi ya nishati safi
ya kupikia iliyopendekezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya
kushiriki mkutano wa 38, Rais Dkt. Samia atashiriki mkutano wa Baraza la Amani
na Usalama la Umoja wa Afrika unaofanyika tarehe 14 Februari 2025.
0 Maoni