WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza matembezi ya amani,
maridhiano na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwataka viongozi wa dini waendelee
kusisitiza amani miongoni mwa waumini wao.
“Viongozi wa madhehebu ya dini endeleeni kuwahimiza waumini
wenu kulinda amani ya nchi yetu. Wafahamisheni waumini athari za kutozingatia
thamani ya amani tuliyonayo huku mkisisitiza wajibu wa kila mmoja kuhakikisha
amani inadumishwa hapa nchini,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumamosi, Desemba 2, 2023) wakati
akizungumza na washiriki na wadau mbalimbali kwenye ukumbi wa Karimjee jijini
Dar es Salaam, mara baada ya kushiriki matembezi hayo kwa km. 5 ambayo
yameratibiwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT).
Pia amewataka viongozi wa dini, washirikiane na Serikali katika
kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na gesi asilia ili kuinusuru
nchi na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini
wawaeleze waumini wao kwamba licha ya mafanikio ambayo Serikali imeyapata
kwenye mapambano dhidi ya VVU, wanapaswa watambue kuwa UKIMWI bado upo.
“UKIMWI bado upo, ninawaomba suala hili lipewe kipaumbele
wakati wa mahubiri, hotuba na mihadhara. Endeleeni kuwakumbusha waumini kuhusu
umuhimu wa kubadili tabia hususan zile zinazochangia maambukizi.”
“Jana ilikuwa ni maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.
Kwenye tathmini yetu, malengo ya 95-95-95 yamefanikiwa kwa maana ya 95 ya
kwanza imeongezeka kwa sababu watu wengi wamejitokeza kupima. Hii inahamasisha
upimaji na watu wanaojitokeza ni wengi lakini wanaopima sana ni wanawake.
Wanaume hamuendi kupima.”
“Wanaume jitokezeni
mkapime, msitegemee matokeo ya wake zenu. Mimi ndiye Balozi wa kuhamasisha
wanaume kupima virusi vya UKIMWI, kwa hiyo msiniaibishe. Kuanzia leo, nendeni
kwenye vituo vyetu mkapime VVU.”
Kuhusu 95 ya pili, Waziri Mkuu amesema hii imefanikiwa kwani
waliopima na kugundulika wanatumia dawa kama inavyoshauriwa na 95 ya tatu
imefanikiwa kwani wanaotumia dawa, kwa asilimia kubwa wamefanikiwa kufubaza
virusi hivyo.
Amewataka viongozi hao wawaangalie zaidi vijana kwani ni
kundi lililo kwenye hatari zaidi. “Kwa kuwa kundi la vijana liko katika hatari
zaidi ya kupata maambukizi, ninawasihi sana imarisheni huduma za unasihi na
malezi yenye mlengo wa kustahimili mabadiliko yanayotokana na utandawazi.
Ninayo imani kuwa, kwa nafasi zenu ndani ya jamii, vijana watawasikia,
watawatii na kubadilika.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuleta mtangamano na kukuza demokrasia. Kaulimbiu ya matembezi hayo ni: “Dumisha Amani, Maridhiano, Upendo na Udugu wa Kibinadamu.”
“Kipekee ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha kunakuwepo na mtangamano wa kisiasa nchini unaojumuisha siasa safi,
za kiustaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu. Kutokana na maono na
jitihada zake, hali ya siasa nchini ni tulivu na vyama vya siasa vinaendelea
kutekeleza majukumu yao ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo
mbalimbali nchini.”
0 Maoni