‘Shetani’ na wenzake wapandishwa kizimbani kwa kosa la mauaji

 

Watu watano akiwemo Mtingwa Kilimanjaro maarufu kama Shetani (42) Mkazi wa Mbamba, wamefikiswa katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza leo Januari 19, 2024 na kusomewa shtaka la mauaji katika kesi namba 1462 ya mwaka huu.

Akisoma shtaka hilo mbela ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Tumsifu Barnabas Mwendesha Mashtaka wa Polisi Mkaguzi wa Polisi Martha Chacha amewataja washtakiwa wengine kuwa ni Majaliwa Damasi, (18) Mkazi wa Masumbwe, Emmanuel  Damasi, (34)  Mkazi wa Bulungwa, Selina Mchele (49) Mkazi wa Lwenge, pamoja na Maneno Mashauri (19) naye Mkazi wa Lwenge.

Martha ameiambia Mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Oktoba 12, 2023 huko Lwenge wilayani Sengerema kwa kumuua Sophia Maduka (61) na mumewe Mathias Lusesa (73) wote wakazi wa Lwenge wilayani humo kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Hata hivyo washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote na kurejeshwa rumande kutokana na Mahakama hiyo kukosa mamlaka kisheria ya kusiliza shauri hilo.

Ikumbukwe taarifa ya kukamatwa kwa washtakiwa hao watano ilitolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza SACP- Wilbroad Mutafungwa Januari 13, 2024 ambapo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Sengerema ASP Tito Mohe akiwa na timu ya makachero walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa mafichoni.

Hakimu Barnabas ameahilisha kesi hiyo hadi Februari Mosi, 2024 kwa ajili ya kutajwa tena.



Chapisha Maoni

0 Maoni