Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA,
Tundu Lissu ameitaka Mahakama Kuu
Masjala ya Dar es Salaam kutoendelea na usikilizaji wa kesi ya uhaini
inayomkabili, kwa kile alichodai kuwa wananchama na wafuasi wa chama hicho
kufukuzwa mahakamani.
Kauli hiyo ya Lissu ameitoa leo Septemba 16,2025, kabla ya
kuanza kwa usikilizaji wa sababu ya pili ya pingamizi lake la kupinga uhalali
wa Mahakama hiyo kuendelea na usikilizaji wa kesi yake.
Kutokana na madai hayo aliyotoa leo, Lissu ameiomba Mahakama
itoe amri ya ahirisho hadi pale wafuasi
wake hao watakaporuhisiwa kuingia katika ukumbi wa Mahakama ili kusikiliza
mwenendo wa kesi yake.
Hata hivyo, hoja hiyo imepingwa na upande wa Jamhuri ikisema
madai ya wafuasi wake kufukuzwa mahakamani, si sababu ya msingi ya kuhairisha
kesi, badala yake mshtakiwa atakuwa amegomea kuendelea na kesi.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imehairisha kesi hiyo kwa muda wa saa moja kwa ajili ya kuandaa uamuzi wake na kutoa maelekezo ya namna ya kuendeleana kesi hiyo.
Hata hivyo baada ya kurejea Mahakama ilitupilia mbali hoja iliyokuwa umewasilishwa na Lissu, ambaye
alidai kuwa Polisi kupitia amri ya ZCO waliwatoa watu (viongozi na wafuasi wa
CHADEMA) waliofika Mahakamani hapo kusikiliza mwenendo wa kesi inayomkabili.
Katika maelezo yake Jaji Ndunguru amesema katika ufuatiliaji
wake Mahakama imebaini hakuna amri yoyote iliyotolewa inayotaka watu watoke
kwenye chumba cha Mahakama
Sambamba na hilo Jaji Ndunguru amesema wakati Majaji
wanaingia waliona baadhi ya watu wakitoka kwenye chumba cha Mahakama na kwamba
kwa wakati huo hawakuona mtu/ watu waliokuwa wakitoa amri ya kuwafukuza.
Mahakama pia imetoa wito kwa wadau wake wote kutambua kuwa
chumba cha Mahakama kina idadi ya watu inayotosheleza, na si kweli kwamba wote
watakaofika Mahakamani wanaweza kutosheleza kuingia kwenye chumba cha Mahakama.
Lakini pia, Mahakama imetoa wito kwa wadau wote kutumia
utaratibu uliotumika juma lililopita ambao ulikuwa rafiki kwa watu wote kufuatilia
bila kikwazo chochote.
Aidha, Mahakama imetaka pande zote na wadau kutafuta suluhu
ya mapema pale inapotokea sintofahamu kama hiyo au ya aina yoyote ile, itafutwe
suluhu kabla Majaji hawajaingia kwenye chumba cha Mahakama.
Baada ya uamuzi huo, sasa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu inaendelea.
0 Maoni