Kiwanda cha Tansalt kilichopo mkoani Tanga kimekuwa msaada
mkubwa kwa wachimbaji na wakulima wa chumvi nchini kwa kusaidia kuwapatia
uhakika wa soko la bidhaa hiyo, hatua ambayo imechangia kuongeza kipato cha
wazalishaji wadogo na kukuza thamani ya chumvi katika masoko ya ndani na ya
kikanda.
Hayo yalibainishwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Tanga,
Mhandisi Laurent Bujashi wakati akizungumza na Madini Diary ambapo alieleza
kuwa, wachimbaji wa chumvi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kuyauza mazao
yao kwa bei ya kusuasua kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.
Hata hivyo, kupatikana kwa Tansalt kumeimarisha mnyororo wa
thamani wa chumvi, kwani kiwanda kinanunua na kuchakata chumvi ghafi kutoka kwa
wachimbaji wadogo wa Tanga na mikoa ya ukanda wa pwani na kuisambaza kwa wingi
katika masoko ya kitaifa na nje ya nchi.
“Mbali na kuongeza thamani ya chumvi, kiwanda hicho pia
kimetoa ajira kwa wakazi wa Tanga na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi,
ikiwemo usafirishaji, biashara ndogo ndogo na huduma za kijamii. Vilevile,
uwepo wa chumvi yenye iodini inayozalishwa na Tansalt umechangia kwa kiasi
kikubwa katika mapambano dhidi ya maradhi yatokanayo na upungufu wa madini ya
iodini nchini.” Alisema Bujashi.
Kwa mujibu wa wadau wa sekta ya chumvi, Tansalt inatajwa
kuwa mfano wa jitihada za Serikali na sekta binafsi katika kuhakikisha
rasilimali za bahari na ardhi zinachangia moja kwa moja kwenye maendeleo ya
wananchi, huku ikihimiza uwekezaji zaidi katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata
chumvi ili kupanua masoko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Badru Issa
Badru alisema kuwa, Kiwanda kinazalisha chumvi kwa matumizi ya nyumbani
(domestic salt), viwandani (industrial salt), pamoja na chumvi yenye madini ya
iodini kwa ajili ya afya ya binadamu (iodized salt).
“Tansalt imejipanga
kuhakikisha wachimbaji na wakulima wa chumvi nchini wanapata soko la uhakika
kwa bidhaa zao. Tunachakata chumvi ghafi kutoka kwao na kuisambaza kwa viwango
vya kitaifa na kikanda, hatua inayoongeza kipato cha wananchi na kuchochea
maendeleo ya uchumi wa Tanga na taifa kwa ujumla. Kiwanda kina uwezo wa
kuzalisha tani 5 hadi 8 za chumvi ndani ya saa moja,” alisema Badru.
Aidha, aliongeza kuwa Tansalt ni moja ya wazalishaji wakubwa nchini, na chumvi yake inasambazwa ndani ya Tanzania na pia kuuzwa kwenye masoko ya Afrika Mashariki.
0 Maoni