Wahandisi kutoka Wizara na Taasisi zinazojihusisha na usimamizi wa miradi ya usafirishji
hususani ile ya miundombinu wapo Mkoani Arusha kwa ajili ya kupatiwa
mafunzo ya kuimarisha usimamizi wa
miradi ili kupunguza gharama na ucheleweshaji wa miradi nchini.
Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Chama
cha Barabara Tanzania (TARA) ambapo wataalamu wabobezi kutoka Tanzania
na Zambia watawasilisha mada mbalimbali
katika kuwajenga uelewa Wahandisi hao.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mgeni rasmi
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri kutoka Wakala ya Barabara za
VIjijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Florian Kabaka amesema kuwa yapo
mapungufu makubwa kwa wataalam hususani
wakati wa mikataba inayopelekea hasara
kwa serikali hivyo mafunzo hayo yatawasadia katika maeneo yao.
“Kumekuwa na matatizo mengi katika mikataba yetu, shida
nyingi kwenye hiyo mikataba ikiwepo mikataba kubadilika ama kuzidi kiwango
tofauti na bajeti zilizowekwa, madai yasiyokuwepo kwenye mikataba ya awali au
kugundulika matatizo mengine yanayotokana na viwango vya kazi kubadilika
kwasababu awali havikuwa vimejadiliwa vizuri na hivyo kupelekea kuipa hasara
serikali," amefafanua.
Amesema kutokana na hali hiyo sekta ya usafirishaji kwa
kushirikiana na TARA wameona ni vyema kufanya mafunzo hayo ili watendaji waweze
kutekeleza mikataba kwa usahihi na ubora kuanzia pale miradi inapobuniwa hadi
utekelezaji wake kukamilika.
Hata hivyo Mhandisi Kabaka ameshauri ni vyema wasimamizi wa
miradi wanaochukuliwa hususan wale ambao hawana uzoefu ni vyema wakawa chini ya
usimamizi wa wabobezi ili kuondokana na uwezekano wa kuiletea hasara serikali.
Naye, Mhandisi Pharles Ngeleja kutoka TARURA amesema kwamba
upo umuhimu wa sekta ya usafirishaji
kukuwa kwa haraka hasa vijijini hivyo wao kama TARURA wameweza kufungua
maeneo mengi hususan ya vijiji kwa kujenga miundombinu ya barabara ikiwemo
madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe.
Amesema tangu kuanzishwa kwa TARURA mwaka 2017
wamefanikiwa kujenga madaraja ya mawe takriban 453 na hivyo kuweza
kuokoa fedha nyingi na vilevile wananchi wameweza kunufaika kiuchumi na kijamii.
“Katika maeneo mengi hivi sasa yamefunguka na hivyo wananchi
wanaweza kufikia huduma za kijamii na kuweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi
na hivyo kuinuka kiuchumi,” amesema.
Mafunzo hayo ya siku tano yamehudhuriwa na wahandisi kutoka OR-TAMISEMI, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Road Fund, TARURA pamoja na TANROADS.
0 Maoni