Kamishna Meing’ataki asisitiza matumizi sahihi ya rasilimali, nidhamu na uwajibikaji

 

Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wametakiwa kulinda na kutumia kwa usahihi rasilimali za Shirika ikiwemo mitambo ya ujenzi, magari ya doria na vifaa vya kiufundi ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta tija katika nyanja za Kiuchumi na kijamii kwa Taifa.

Wito huo ulitolewa jana Septemba 15, 2025 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Godwell Meing’ataki, wakati alipoongoza kikao kazi cha Menejimenti ya Hifadhi za Taifa Kanda ya Kusini iliyohusisha Hifadhi za Taifa Kitulo, Ruaha na Katavi, kikao kilichojadili changamoto na mikakati ya kuimarisha utendaji katika hifadhi hizo.

Kamishana Meing’ataki alisisitiza pia nidhamu kwa Maafisa na Askari wa uhifadhi,alisema TANAPA inasimama juu ya misingi ya uadilifu, utiifu na heshima ya kiutumishi, hivyo nidhamu ndiyo msingi wa kulinda taswira ya Shirika na nchi kwa ujumla.

Aidha, aliwataka wakuu wa Hifadhi za Kitulo, Ruaha na Katavi kuhakikisha wanawasimamia kikamilifu watumishi walioko chini yao kwa kuzingatia sera na miongozo ya uwajibikaji ya Shirika, ameonya pia kiongozi asiyetekeleza wajibu wake atalazimika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Katika kikao hicho pia, ushirikishwaji wa watumishi na ubunifu ulisisitizwa kama njia ya kuongeza tija, kukuza mapato ya utalii na kuleta manufaa kwa Serikali pamoja na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi.

kikao hicho  ni mikakati ya Shirika ya kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi  huku kikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuzitangaza Hifadhi za Taifa kiutalii, ili na Hifadhi za Kanda ya Kusini ziendelee kukua na kutoa mchango mkubwa kwa Taifa kama ilivyo kwa hifadhi nyingine nchini.




                        Na: Happiness Sam - Mbeya

Chapisha Maoni

0 Maoni