Mahakama ya Wilaya ya Rungwe imemhukumu Tecla Lumala (24),
mkazi wa Morogoro, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya
kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 18, 2025 na Hakimu wa Mahakama
ya Wilaya ya Rungwe, Mhe. Mwinjuma Bwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi
uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, Tecla alikamatwa Desemba
22, 2024 akiwa anasafirisha kiasi cha kilogramu 6.8 za bangi kupitia kizuizi
cha polisi cha Kayuki (Police Road Block) kilichopo katika Kijiji cha
Ngujubwaje "A", Kata ya Ilima, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani Januari 1, 2025 na
kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Bwanga, ambapo alitiwa hatiani kwa kosa la
kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Akisoma hukumu hiyo, Mhe. Bwanga alisema kuwa Mahakama
imezingatia uzito wa kosa na madhara ya dawa za kulevya kwa jamii, hivyo adhabu
ya kifungo cha miaka 30 jela ni ya haki na itatumika kama fundisho kwa wengine.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea
kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi
katika mashauri mbalimbali yanayowakabili watuhumiwa wa makosa ya jinai, ili
kusaidia upatikanaji wa haki kwa mujibu wa sheria.
Aidha, jeshi hilo limewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki kisheria.
0 Maoni