Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza Watanzania
wote kupuuza taarifa za upotoshaji zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii,
zenye lengo la kuwachochea kuondoa fedha zao benki na kuzihifadhi majumbani.
Katika taarifa iliyotolewa karibuni jijini Dar es
Salaam na kusainiwa na Gavana wake, Bwana Emmanuel M. Tutuba, Benki Kuu
imesisitiza kuwa taarifa zinazodai kuwa Benki Kuu inachapisha fedha kwa ajili
ya kugharimia uchaguzi, au kwamba baadhi ya benki za biashara zimeishiwa fedha,
ni za uongo na za uzushi kabisa.
"Napenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa
taarifa hizo siyo za kweli, zinapaswa kupuzwa na kukemewa wote wanaoupotosha
umma kuhusu hili jambo. Tunawasihi wananchi kutokushawishika kutoa fedha zao
kutoka kwenye mabenki," ilisema taarifa hiyo.
Uchapishaji Fedha ni Kisheria
Benki Kuu imefafanua kuwa, kama ilivyo kwa benki
nyingine duniani, inachapisha fedha kwa mujibu wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya
Benki Kuu, Sura 197. Fedha hizo huwekwa kwenye mzunguko kulingana na shughuli
za kiuchumi na mahitaji ya kubadilisha fedha zinazochakaa.
Kinyume na uchochezi huo, Benki Kuu imetoa takwimu
thabiti kuonyesha utulivu na ustawi wa Sekta ya fedha:
Akiba ya Fedha za Kigeni: Imeongezeka hadi Dola za
Marekani bilioni 6.7. Kiasi hiki kinatosha kuagiza bidhaa nje ya Nchi kwa
kipindi cha miezi 5.4, ikilinganishwa na lengo la miezi 4.0.
Ukwasi na Mtaji: Viwango vya utoshelevu wa mtaji na
ukwasi kwenye benki zote za biashara viko juu zaidi ya viwango vinavyotakiwa
kisheria, ikiwa ni uthibitisho wa uthabiti wa sekta hiyo.
Hatari ya Kuzihifadhi Nyumbani
Benki Kuu imewaonya wananchi kuhusu hatari za
kuondoa fedha na kuzihifadhi majumbani, ikisema kuwa hatua hiyo inawaweka
katika hatari ya wizi, kupotea, kutumiwa vibaya, au uharibifu kutokana na
majanga kama moto.
"Kutokana na mazingira hayo mazuri ya kiuchumi
na kifedha nchini, uamuzi wa kuondoa fedha kutoka benki na kuzitunza nyumbani
haufai kwa kuwa ni utamaduni wa kizamani wenye hatari nyingi ikilinganishwa na
kuibwa, kuvutiwa wezi wanaoanza kukudhuru, kupotea, kuzitumia vibaya katika
shughuli zisizokusudiwa," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
BoT imeongeza kuwa, uamuzi wowote wa kuondoa fedha
benki na kuzihifadhi nyumbani unakinzana na juhudi za Serikali za kukuza
matumizi ya mifumo rasmi ya kibenki.
Gavana Tutuba amewahimiza wananchi wote kuendelea kutumia
huduma za benki bila wasiwasi wowote, na kuwataka wanaofanya upotoshaji huo
kutambua kuwa wanachelewesha juhudi za Taifa za kuimarisha utulivu wa Sekta ya
fedha nchini.

0 Maoni