Kadiri Taifa linavyojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 29, 2025, jukumu la viongozi wa dini limekuwa muhimu zaidi kuliko wakati
mwingine wowote. Tanzania, inayojulikana kwa amani, umoja na tofauti za
kitamaduni, ina jukumu la kihistoria la kuendelea kuwa mfano wa upendo na
utulivu barani Afrika.
Kwa kuwa zaidi ya asilimia 99 ya Watanzania ni
waumini wa dini mbalimbali, Waislamu, Wakristo na imani za asili, viongozi wa
dini wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha maelewano na mshikamano vinadumu.
Dini inaweza kuwa nguvu ya umoja, si chachu ya mgawanyiko.
Tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, maelewano ya kidini yamekuwa nguzo ya amani ya Taifa. Mwalimu
alisisitiza ujamaa na usawa, akijenga misingi ya kuheshimiana bila kujali dini.
Hata katika miaka ya 1990, wakati Tanzania ilipokuwa
inapitia mabadiliko kuelekea mfumo wa vyama vingi, viongozi wa dini waliongoza
juhudi za kudumisha mazungumzo badala ya migogoro, wakisaidia Nchi kuepuka
machafuko yaliyotokea katika mataifa jirani.
Lakini leo, tunashuhudia sauti za wachache
mitandaoni zikihamasisha vurugu, migawanyiko na maandamano yasiyo na msingi.
Sauti hizi za chuki haziwakilishi Watanzania wengi wanaotamani uchaguzi wa
amani na ushiriki wa kidemokrasia.
Katika kipindi hiki wadau wengi wameonya kuwa
mtazamo wa kuona Amani na Haki kama vitu vinavyopingana unaweza kuhatarisha
umoja wa kitaifa.
Viongozi wa dini wamehimizwa kutumia ushawishi wao
kuhakikisha kuwa nyumba za ibada zinabaki kuwa vituo vya sala na umoja, na si
majukwaa ya kueneza migawanyiko ya kisiasa.
Wito huu unasisitizwa na kauli za vitabu vitakatifu:
Qur’an (49:9) "Fanyeni amani kati yao," na Zaburi (34:14)
"Tafuteni amani na kuifuata," zikikumbusha kwamba Amani ni wajibu wa
kimsingi wa kiimani.
Licha ya wito huo, kumekuwa na maoni makali kutoka
kwa wananchi wakisema kwamba Amani bila Haki si zaidi ya 'Uvumilivu' na kwamba
viongozi wa dini wanakwepa wajibu wao wa kuitetea Haki kwanza.
Utamaduni wa Kistaarabu: Kupingana Bila Kupigana
Wakati mjadala huu ukiendelea, wataalamu wa jamii na
siasa wanasisitiza kuwa mchango mkuu wa Taifa la Tanzania kwa dunia ni
kuendeleza utamaduni wa kistaarabu wa kupingana bila kupigana.
"Maendeleo ya kweli, kama alivyosema Mwalimu
Nyerere, yanatokana na maelewano, si migogoro. Sisi kama Taifa, tunapaswa
kuelewa kwamba kuna haja ya kutoa maoni tofauti, kukosoana, na kudai haki,
lakini yote haya yafanyike ndani ya utaratibu wa kisheria na bila kuhatarisha
uhai na ustawi wa mwenzetu," alisema mmoja wa wataalamu hao.
Wito mkuu kwa viongozi wote wa dini na wa kisiasa,
pamoja na wananchi, ni kutumia sanduku la kura kama daraja la amani, na si bomu
la migawanyiko. Uchaguzi unapaswa kuwa fursa ya kudumisha umoja, huku wananchi
wote wakihamasishwa kutojihusisha na miito yoyote ya vurugu au machafuko
inayoenezwa hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Amani na Haki ni nguzo mbili zinazoweza kufanya kazi
pamoja, na si lazima zipingane. Wajibu wetu sote ni kuhakikisha kwamba kupitia
mjadala wenye staha na utaratibu wa kisheria, tunajenga Tanzania yenye ustawi
na maendeleo yanayoambatana na utulivu kwa vizazi vijavyo.

0 Maoni