Imeelezwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
amewezesha kuwasha umeme vijiji vyote 368 sawa na asilimia 100 na sasa
utekelezaji unaendelea kwa kasi ya kupeleka huduma ya umeme kwenye vitongoji
vyote ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo
jijini Arusha.
Hayo yamebaibishwa leo Agosti 28, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi
ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu,
wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, sambamba
na kuzungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA ambapo ameweza
kushuhudia wananchi wakiunganishiwa huduma ya umeme Wilaya ya Arumeru,
Kitongoji cha Kisongo Juu jijini humo.
Ameongeza kuwa, mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji
unaendelea vizuri ambapo vitongoji 936
kati ya vitongoji 1,505 hadi sasa tayari vimeunganishwa na nishati ya
umeme na kazi hiyo inaendelea kwa kasi ili kumaliza kwa wakati na wananchi
waweze kunufaika na uwepo wa nishati ya umeme katika maeneo yao.
"Tumshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa namna mbavyo
anaendelea kuwezesha sisi REA kuweza kutekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye
vitongoji kwa kasi kubwa kama mnavyoiona katika mkoa huu wa Arusha na wananchi
wengi wanaendelea kuunganishiwa umeme, " amesema Mhe. Balozi Kingu.
Vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea
kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa huu inayolenga kuwapatia huduma za uhakika
za nishati ili kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi katika maeneo yote ya
vijijini.
Katika hatua nyingine, Mhe. Balozi Kingu amehaidi kuwa, REA
itaendelea kuwafikishia huduma ya umeme wananchi kwenye vitongoji na maeneo ya
pembezoni ya miji ili kuwawezesha kuwa na umeme wa uhakika katika maeneo hayo
na kuwezesha kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kisongo Juu Adam William, amesema mradi huo wa umeme katika eneo hilo ni fursa kwao kuweza kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kusaga mahindi na mpunga kwa kutumia mashine ya umeme, kuchaji simu na fursa nyingine za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa nishati ya umeme.
0 Maoni