Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi wa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dkt. Athumani
Kihamia, na kumteua Said Habibu Tunda kushika nafasi hiyo.
Katika
mabadiliko hayo, Rais Dkt. Samia pia ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Bw. Waziri Kindamba, na kumteua Pius
Andrew Ng'ingo kushika nafasi hiyo.
Mabadiliko
hayo yanakuja wakati huduma ya mabasi ya mwendo kasi ikikumbwa na changamoto
mbalimbali, ikiwemo ucheleweshaji wa huduma, msongamano wa abiria vituoni,
pamoja na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa watumiaji wa mfumo huo.
Wakati
huo huo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewateua David Kafulila na Ramadhan Dau kuwa
wenyeviti wa bodi za Wakala na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka.
Taarifa
iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka imesema Rais
Samia amevunja Bodi za Wakala na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka na kuwateua
Dau na Kafulila kuwa wenyeviti wapya.
Taarifa
hiyo imesema Kafulila ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri yaWakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Dau ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).
Huduma ya
mabasi yaendayo haraka imekuwa mojawapo ya miradi muhimu ya usafiri jijini Dar
es Salaam, lakini kwa muda sasa imekuwa ikilalamikiwa kwa kukosa ufanisi
unaotarajiwa, jambo ambalo limekuwa likiibua maswali kwa wadau mbalimbali wa
sekta ya usafiri.
0 Maoni