Mkazi wa
Nyakato ambaye ni Mfanyakazi wa ndani (Hauseboy), Fred Kelendo Marekioli (19),
amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kwa tuhuma za
kumfanyia shambulio la aibu mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 5 (jina
limehifadhiwa kwa sababu za kisheria).
Akisoma
hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Ramla Shehagilo, Wakili
wa Serikali, Tunu Msangi ameieleza mahakama hiyo kuwa tukio hilo lilitokea
Septemba 9, 2025 katika eneo la Mwananchi jijini humo, ambapo mshtakiwa
anadaiwa kutenda kitendo hicho cha ukatili dhidi ya mtoto huyo mdogo.
Katika
kesi hiyo ya jinai yenye namba 22967/2025, mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja
la shambulio la aibu, kinyume na Kifungu cha 138C (1)(d)(2)(b) cha Sheria ya
Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
Hata
hivyo, mshtakiwa amekana shtaka hilo, huku hakimu Shehagilo anayesikiliza kesi
hiyo akieleza kuwa, kosa hilo linadhaminika kwa masharti, ikiwemo kuwa na wadhamini
wawili wenye vitambulisho halali vya taifa, barua za utambulisho kutoka
Serikali ya Mtaa na kila mdhamini kusaini hati ya dhamana ya shilingi milioni
moja.
Mshtakiwa
ameshindwa kukidhi masharti ya dhamana jambo lililosababisha kurudishwa rumande
hadi leo Septemba 23, 2025, kesi hiyo itakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa
kusomewa hoja za awali.
0 Maoni