MGOMBEA
urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
amesema tofauti ya chama hicho na vyama vingine ni kuwa CCM inapoahidi
inatekeleza huku ikijua itatekeleza vipi na wapi itapata fedha za utekelezaji.
Dkt.
Samia ameyasema hayo jana Septemba 22, 2025 kwenye Viwanja vya VETA Msamala
wilayani Songea mkoani Ruvuma alipohutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza
kusikiliza Ilani ya chama hicho katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Akiwa na
mgombea mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Dkt. Samia amesema wananchi wana
kila sababu ya kukichagua tena Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuongoza nchi
kwakuwa kinaahidi na kinatekeleza.
"Kuna
watu wanazunguka kama mimi wakisema ilani zao, lakini kila nikiwasikiliza ni
yaleyale yaliyopo kwenye ilani ya chama chetu, lakini ndani ya ilani ya Chama
Cha Mapinduzi, tukiandika huku tukijua tutatekeleza kwa njia gani, fedha
itatoka wapi, vipi tutakamilisha tuliyoyaandika. Suala siyo kusema tutafanya
lakini vipi tutafanya hilo ndilo suala muhimu," ameeleza Dkt. Samia.
Ameongeza
kuwa "CCM tunasimama na kujiamini kwa ujasiri mkubwa kuomba kura mtuchague
tuendelee kuongoza serikali hii kwa sababu tumefanya nanyi mmeona na ninaamini
tutafanya tena na mtaona".
Mbali ya
kumsifu Dkt. Nchimbi ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma kuwa ana sifa za
uongozi, Dkt. Samia ameahidi kuifungua Mikoa ya Kusini kuwa kitovu cha biashara
na maendeleo.
Akiwa
katika mikutano ya kampeni Songea Mjini, Namtumbo na Tunduru mgombea huyo
ameainisha uwekezaji utakaofanywa na serikali yake katika kuchochea upatikanaji
wa ajira kwa vijana.
Amesema
katika hatua za maendeleo mikakati ya serikali yake ni kuufungua Mkoa wa Ruvuma
na mingine ya Kusini kuwa kitovu cha biashara.
Amesema
serikali yake itajenga kilometa 1,000 za reli ya kisasa itakayounganisha Mikoa
yq Mtwara na Ruvuma na kurahisisha usafirishaji wa madini yatakayochimbwa
Mchuchuma na Liganga.
Ameongeza
kuwa, serikali yake itaboresha Kiwanja cha Ndege cha Songea na ujenzi wa
Bandari ya Mbamba Bay ambao umefikia asilimia 35.
Pia
amesema, serikali imekamilisha ujenzi wa Bandari ya Ndumbi ambayo imechochea
biashara baina ya Tanzania na Malawi kupitia Nkata Bay hivyo kuongeza fursa za
kiuchumi katika Ziwa Nyasa.
"Tunafungua
ukanda wa kusini lengo likiwa biashara zifanyike kwa kutumia anga, barabara na
maji ili Ruvuma iwe kitovu kikubwa cha biashara," ameeleza.
Dkt.
Samia alisisitiza ahadi yake ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kidatu -
Ifakara - Malinyi hadi Lumecha inayounganisha Mikoa ya Ruvuma na Morogoro
ambayo pia itachochea biashara.
Ameahidi
kujenga na kukamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha tawi la Songea
na kujenga chuo cha ufundi cha walemavu Liganga.
Pia
amesema serikali imetekeleza mradi wa ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhia mazao
Mkoani Ruvuma.
Dkt.
Samia ameahidi kuendeleza kutoa kipaumbele uchimbaji salama kwa wachimbaji
wadogo.
Aidha
amesema, wataendelea na mradi wa kuchimba madini ya Uranium na kuwa lengo la
Serikali yake ni madini hayo yachakatwe na yasafishwe ndani ya nchi.
Pia
ameahidi, kujenga barabara ya mchepuko kupunguza msongamano wa magari katikati
ya mji wa Songea.
Leo Dkt. Samia anamalizia kampeni mkoani Ruvuma akiwa Nakapanya halafu anaingia Mtwara akianzia kampeni Nanyumbu na Masasi.
Na. Aboubakary Liongo - Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM
0 Maoni