WAZIRI
MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo ya
uchumi nchini ambapo katika mwaka 2022 sekta hiyo imekua kwa asilimia 10.9 na
kufikia mchango wa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa mwaka 2024,
ikilinganishwa na asilimia 9.0 mwaka 2023.
Ametoa
kauli hiyo jana Septemba 22, 2025, wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Nane ya
Teknolojia ya Madini Mkoa wa Geita, yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
Amesema
kuwa hatua hiyo imetokana na jitihada mbalimbali za Serikali ya awamu ya sita
ikiwemo kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa biashara
ya madini, matumizi ya mifumo ya
kielektroniki (online mining cadastre system), uwepo wa masoko ya madini na
ufuatiliaji wa mikataba ya uwekezaji.
"Serikali
ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye
sekta ya madini ili rasilimali za madini zichangie kwa katika ukuaji wa uchumi
na ustawi wa Watanzania wote".
Waziri
Mkuu ametoa rai kwa wadau wa sekta ya madini kuendelea kuwekeza katika
teknolojia kwani ndiyo daraja la mageuzi kuanzia utafiti na uchimbaji,
usafishaji na biashara ya madini. "Bila teknolojia sahihi, haiwezekani
kuongeza tija, kuhakikisha usalama wa wachimbaji, kulinda mazingira, wala
kufanya uongezaji thamani wa madini yetu".
Ameongeza
kuwa kupitia maonesho hayo, katika kiipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 Wachimbaji
wadogo wa Geita wamezalisha zaidi ya kilo 22,000 za dhahabu zenye thamani ya
Shilingi Trilioni 3.44, huku Serikali ikipata zaidi ya Shilingi Bilioni 235.5
kama mrabaha. "
Aidha,
makampuni makubwa kama Geita Gold Mine na Buckreef katika kipindi hicho wamezalisha
kilo 76,530 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Trilioni 11.38, na Serikali
kupata zaidi ya Shilingi Bilioni 793 kama mrabaha."
Kwa
Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa
Tanzania sasa imepiga hatua kwa kuwa na viwanda vya kutengeneza zana mbalimbali
za uchimbaji wa madini.
"Katika
mwaka wa fedha 2024-2025 tumeweza kuzalisha tani 62 za dhahabu tofauti na nyuma
tulikuwa tukizalisha tani 40-50 kila mwaka hii inatufanya Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi tano bora Afrika katika uzalishaji wa dhahabu."
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema huo umefanya kazi kubwa ya
kusambaza umeme vijijini na kwa kuwa kazi ya uchimbaji unahitaji umeme tayari
umeme umepelekwa katika maeneo mengi ya wachimbaji wadogo.
"Tumefanyia
kazi maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupeleka umeme
katika maeneo ya wachimbaji wadogo ili wafanye kazi zao na kuwa na uzalishaji
wa uhakika katika maeneo yao."
0 Maoni