Wataalamu
kutoka kutoka Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Idara ya Misitu na Nyuki na
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) wamefanya ziara nchini Ufini kujifunza kuhusu
namna bora ya kushirikisha sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya misitu
nchini. Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ubalozi wa Ufini nchini Tanzania ni
sehemu ya juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii za kubadilishana uzoefu kati
ya wataalam wa Tanzania na wale wa Ufini juu ya ushirikishwaji sahihi wa sekta
binafsi katika uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali misitu.
Akizungumzia
wakati wa ziara hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dkt Tuli S. Msuya
alisema kuwa ziara hiyo itasaidia utekelezaji wa Mkakati wa TaFF wa Utafutaji
Fedha (Fundraising Strategy) wenye lengo la kutanua wigo wa vyanzo vya mapato
ili kuongeza uwezo wa TaFF kujiendesha iwapo vyanzo vya sasa vinavyotokana na maduhuli
ya misitu havitakuwepo.
“Tumejifunza namna bora ya ushirikishwaji na
uwezeshaji wa sekta binafsi katika mnyororo mzima wa shughuli za uhifadhi,
uendelezaji na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu katika kuchangia
ongezeko la kipato cha jamii na Uchumi wa nchi. Mafunzo hayo pia yanatoa fursa
kwa TaFF kuanzisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa Ufini katika
ushirikishwaji na uwezeshaji wa sekta binafsi nchini,” aliongeza Dkt. Msuya.
Naye,
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Misitu na Nyuki Bw. Seleboni J. Mushi, alisema
kuwa mafunzo hayo yana faida kwa maendeleo ya misitu nchini kwa sababu eneo
lenye misitu ni zaidi ya asilimia 40 ya ardhi ya Tanzania, lakini mchango wake
katika pato la Taifa bado ni mdogo (takribani asilimia 4 tu). Hivyo, ni muhimu
kuhamasisha sekta binafsi ili iongeze ushiriki katika mnyororo wa shughuli za
misitu na kutumia teknolojia ambazo zinaongeza uzalishaji na matumizi sahihi ya
mazao ya misitu. Aidha, sekta binafsi inaweza kuwekeza katika huduma za utalii
na kuongeza pato la taifa na ajira kama inavyofanyika nchini Ufini ambapo idadi
ya Watalii ni takribani watu milioni 8 kwa mwaka.
Washiriki
wengine kutoka TaFF na Ofisi ya Msajili wa Hazina walisema kuwa ziara hiyo ya
mafunzo itasaidia kuendeleza shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali
misitu nchini Tanzania kwa kuangalia utaratibu mzuri wa kuwezesha sekta binafsi
ili zishiriki katika uwekezaji kwenye teknolojia zenye tija katika uvunaji na
uchakataji wa mazao ya misitu nchini Tanzania.
Walioshiriki
ziara hiyo ya mafunzo ni Bw. Seleboni J. Mushi, Mkurugenzi Msaidizi - Maendeleo
ya Misitu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii; Dkt. Tuli S. Msuya, Kaimu Afisa
Mtendaji Mkuu wa TaFF; Dkt. John R. Mbwambo, Mkuu wa Kitengo cha Miradi na
Mipango - TaFF; Bi. Emiliana M. Mallya, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu -
TaFF, na Wenceslaus B. Myanjamu kutoka OTR.
0 Maoni