Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inasisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha uthabiti wa kukabiliana na dharura za afya ya umma barani Afrika.
Makamu wa
Rais amesema hayo wakati akishiriki katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliyofanyika
pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York
nchini Marekani.
Amesema
Tanzania imedhamiria kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kuimarisha
masuluhisho ya kibunifu ya ufadhili pamoja na kuunga mkono mipango ya kikanda
ambayo inapunguza utegemezi wa misaada kutoka nje, na hivyo kuhakikisha kuwa
vipaumbele vya afya vya Afrika vinashughulikiwa na serikali za Afrika.
Aidha,
Makamu wa Rais amesema uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu, na
bidhaa nyingine muhimu za matibabu ni muhimu katika kujitegemea kweye sekta ya
afya. Amesema Tanzania inahimiza uwekezaji katika viwanda vya ndani, mamlaka ya
udhibiti ya pamoja barani kote, na ubia wa uhawilishaji wa teknolojia ili
kuimarisha uwezo wa Afrika wa kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na
zijazo.
Amesema
kufuatia uzoefu wa hivi karibuni wa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza,
ikijumuisha Marburg na vimelea vingine vinavyoambukiza, yametoa hitaji la
kujiandaa kwa nguvu na mifumo ya kukabiliana na maradhi. Ameongeza kwamba
Tanzania inasaidia vitengo vya matibabu ya magonjwa ya kuambukiza, upelekaji wa
haraka wa timu za dharura, na uwekezaji katika miundombinu ya wafanyikazi na
afya.
Pia
amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma, ikiwa
ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, udhibiti wa maambukizi, vifaa,
na uratibu kwa ajili ya kukabiliana na milipuko kwa wakati na kwa ufanisi.
Pia,
Makamu wa Rais ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Nchi
Wanachama wa Umoja wa Afrika, Jumuiya za kiuchumi za kikanda, na Kituo cha
Udhibiti wa Magonjwa cha Afrika ili kuwa na mbinu ya pamoja ya kukabiliana
dharura za afya. Amesema ushirikiano katika uchunguzi, sera na mipango ya
pamoja ya kujenga uwezo itaimarisha uwezo wa pamoja wa kuzuia, kugundua na
kukabiliana na vitisho vya afya vinavyojitokeza.
Mkutano
wa Kamati hiyo umelenga kujadili masuala yanayohusu Kituo cha Kudhibiti Maradhi
Afrika (Africa CDC), chini ya kauli mbiu isemayo ‘Kuhakikisha Uhuru wa Afya
Afrika: Uongozi wa Kisiasa kwa Ufadhili Endelevu wa Sekta ya Afya, Uzalishaji
wa Ndani na Maandalizi dhidi ya Milipuko ya Maradhi.
0 Maoni